Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: MFANYABIASHARA na mmiliki wa kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama, amempongeza Rais Samia Hassan Suluhu, kwa hotuba yake ambayo aliitoa alipokutana na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam.
Msama ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa imeweza kugusa makundi yote.
Mkurugenzi huyo amesema Rais katika hotuba yake hiyo amezungumza mengi na yenye kuliponya taifa kutoka hapa lilipo.
“Kwa mliofuatilia Rais hakuna mahali ambapo hajagusia,hivyo mwenye macho aone na mwenye masikio na asikie,”amesema Msama.
Kwa mujibu wa Msama, hakuna kiongozi anayependa wananchi wake waishi kwa shida na bila amani.
“Hata ukirudi nyuma ukisoma maandiko yote aliyekiuka maagizo ya mfalme kwa ajili ya taifa alichukuliwa hatua kali sana na ndivyo ilivyo hata leo hakuna kiongozi anaweza kubali mtu kukiuka maagizo ya taifa.
“Hivyo natoa rai kwa wazee,wazungumze na watoto wao na wajukuu zao wahakikishe hawadanganywi na walio mataifa ya nje kwa kuwa wao wapo huko na watoto wao wanaishi kwa amani,”amesema Msama.
Aidha aliwaomba vijana kuacha kutumika,kwa kile alichoeleza kuwa kuna ambao hawaitakii mema nchi hii na mwisho wa siku wao ndio watakaoumia na kupata shida.
“Kuna usemi usemao asiyefunzwa na wazazi hufunzwa na ulimwengu ambapo katika harakati za kuvunja sheria kuna vyombo mbalimbali vya dola vitashughulika na nae wakiwemo Jeshi la Polisi,”ameeleza.
Kwa upande wa viongozi wa dini, Msama amesema Mungu hajawatuma kuhubiri siasa bali kuhubiri dini na kukemea maovu.
Kutokana na hilo aliwashauri kama huwataki kuwa watumishi wavue hayo majoho ya kitumishi na kwenda kwenye vyama vya siasa.
“Viongozi wa dini acheni kutuharibia nchi kwani, tunataka kuona wanachi wakienda kwenye nyumba za dini kumtukuza Mungu wao na walio na shughuli nyingine kama biashara wakafanye pia.
“Kwa upande wa wanaharakati wanaotetea haki za binadamu,amewataka nao wawasihi watu kutii sheria za nchi ili kuepuka kuingia katika mikono ya dola.
“Watanzania wenzangu ,tusikubali kutumika hatuna nchi nyingine ya kwenda hivyo tuipende nchi yetu na tuipende Tanzania yetu,”amesisitiza Msama.

