Na Mwandishi Wetu
DODOMA: MKUTANO Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), unatarajiwa kumpata mrithi wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Abdulrahman Kinana.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla, amesema hayo leo, Januari 7, 2025 jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa Habari, ameongeza kuwa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Januari 18 na 19, mwaka huu jijini Dodoma.
Amesema nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti Taifa, iliyoachwa wazi na Kinana, mrithi wake atachaguliwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu huo unaotarajiwa kufanyika.
Makalla amesema kabla ya Mkutano Mkuu, kutakuwa na vikao vya Kamati Kuu ya CCM vitakavyofanyika Januari 16, mwaka huu, kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano Mkuu
Julai 29, mwaka jana Kinana alijiuzulu wadhifa huo baada ya kuomba mara kadhaa kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan ambaye aliridhia ombi hilo.