Na Lucy Lyatuu
SERIKALI imesema iko mbioni kutengeneza mpango wa taifa wa teknolojia ambao utapambanua mahitaji ya teknolojia yalivyo ili kwamba vijana waweze kuleta bunifu zenye kujibu mahitaji ya jamii.
Kaimu Katibu Mkuu, kutoka Wizara ya Elimu Sayansi Na Teknolojia, Ladislaus Mnyone amesema hayo wakati akitoa zawadi na vyeti kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Carolyne Nombo, amesema mpango huo katika miaka 10-3 ijayo utaongeza fursa na kusaidia wabunifu kulitoa taifa kutoka hatua moja hadi nyingine hususani kwenye eneo la ubunifu.
Amesema nchi ya Tanzania ina vituo vya umahiri 12 na kuwataka wabunifu kutoka DIT kuvitumi katika kushiriki kwenye masuala mbalimbali ili waweze kulelewa.
Amewataka vijana kutumia vizuri fursa ya vituo vya umahiri vilivyopo nchini ili kuleta chachu ya maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.

Kuhusu Taasisi hiyo kuwatambua wale waliofanya vizuri amesema ni moja ya eneo linawezesha kuzalishwa kwa wingi teknolojia ambao zitatatua mahitaji yaliyopo katika jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo, Profesa Preksedis Ndomba amesema chuo hicho hutoa zaidi za aina mbili kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo yao ambayo hutoa chachu kwao ili kuongeza bidii.
Amewataka wanafunzi hao ambao wanamaliza masomo yao kuwa kadri watakavyokuwa wakijionesha kwa wadau wao katika utendaji wao ndio hatua mojawapo ya kutangaza ubunifu na huduma wanayotoa.
“Hapa tunawapa cheti na zawadi za kuwatambua lakini haimaanishi kuwa katika Maisha ndio mnatambulika kuwa bora, jambola msingi ni kwamba huduma mnayotoa ndiyo itakayowatangaza,” amesema Profesa Ndomba.

Amewataka wanafunzi wanaosoma DIT kuzingatia maelekezo kutoka kwa walimu na zaidi kuwa na nidhamu, uchapakazi na ustahimilivu ili kuwa na mchango kwa Taifa.

