Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango, amesema maandalizi ya uchaguzi mkuu wa haki, huru na wazi yanaendelea vizuri nchini Tanzania
Hivyo ametoa mwaliko kwa SADC kutuma timu ya waangalizi kwa uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba , mwaka huu2025.

Akihutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama jijini Antananarivo, Madagascar, leo Agosti 16, 2025, Dkt. Mpango amesema kuwa anaiwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.
Ameeleza katika kipindi cha uenyekiti wa Tanzania kwenye Asasi hiyo, mafanikio mbalimbali yamepatikana, yakiwemo kudumishwa kwa utulivu katika ukanda wa SADC, isipokuwa eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako juhudi za kutafuta suluhu zinaendelea.
Amesema jitihada hizo zinajumuisha majadiliano kupitia Mpango wa Luanda na Nairobi, pamoja na hatua zilizopitishwa na mikutano ya pamoja ya EAC na SADC.
Kupitia mikutano hiyo, jopo la Wazee wa Hekima limeundwa, timu za wataalamu kutoka EAC, SADC na AU zimeunganishwa, na utaratibu wa kushughulikia mgogoro huo umetayarishwa.
Amesisitiza kuwa suluhu za migogoro barani Afrika zinapaswa kuongozwa na Waafrika wenyewe, kwa dhamira na kujitoa kwa dhati.

Almeongeza kuwa Tanzania, katika kipindi cha uongozi wake, imeongoza programu mbalimbali za kuzuia na kusuluhisha migogoro, kupeleka vikosi vya kulinda amani kwenye maeneo yenye migogoro,
Pamoja na kuimarisha taasisi za kidemokrasia. Vilevile imeongoza timu za waangalizi wa uchaguzi katika nchi za Botswana, Namibia, Mauritius na Msumbiji.
Amehitimisha kwa kusema kuwa Tanzania imejitahidi kuhakikisha ukanda wa SADC unasalia kuwa salama na tulivu, na kuahidi kuendeleza ushirikiano na mwenyekiti mpya wa Asasi hiyo, Malawi.