Na Danson Kaijage
DODOMA: MAKAMU wa Rais. Dkt.Philip Mpango amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Korea katika kubadilishana wafanyakazi,.
Dkt. Mpango amesema hayo alipofanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania, Eunju Ahn, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Februari 19, 2025.
Katika eneo hilo la kubadilishana wafanyakazi, Dkt. Mpango alimwomba Balozi huyo kuwezesha mchakato wa kujiunga katika Mfumo wa Vibali vya Ajira (EPS) ili wafanyakazi wa Tanzania waweze kuingia katika soko la ajira la Korea.

Mpango amesema huko watanzania watafanya kazi mbalimbalii katika sekta za ujenzi wa meli, sekta ya viwanda na kilimo cha kisasa.
Kwa upande mwingine Dkt. Mpango ameipongeza Jamhuri ya Korea kwa kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya Elimu, Miundombinu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Afya, Kilimo, Viwanda na Nishati.
Amesema makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika madini ya kimkakati yataleta manufaa mengi zaidi kwa kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini mengi ambayo yanaenda sambamba na mwelekeo wa dunia ya sasa ambayo inajikita katika uchumi wa teknolojia za kijani.

Pia Makamu wa Rais amemweza Balozi wa Jamhuri ya Korea umuhimu wa kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Korea yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Halikadhalika amesema ushirikiano unahitajika katika Elimu na kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya kwa kuwapatia mafunzo katika ubingwa na ubobezi wa utoaji matibabu mbalimbali.
Amesema ni muhimu wawekezaji na wafanyabiashara wa Korea kutembelea Tanzania mara kwa mara ili kujionea fursa zilizopo na kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda.
Amesema uongezaji wa thamani kwa malighafi hapa hapa nchini utachochea biashara, uhamishaji teknolojia pamoja ongezeko la ajira kwa wananchi wa Tanzania.

Makamu wa Rais pia amesisitiza kushirikiana katika masuala ya utamaduni, michezo na lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Balozi huyo, Eunju Ahn amesema katika kipindi atakachohudumu nafasi ya Ubalozi nchini Tanzania, atahakikisha anasimamia na kuharakisha kukamilika kwa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa.