Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU – T), Juliana Mpanduji amesema kukosekana kwa sehemu za maegesho kwa boda boda na bajaji ni mojawapo ya changamoto inayoikabili sekta hiyo ya usafirishaji.
Mpanduji amesema hayo wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utafiti kuhusu waendesha Pikipiki Wanawake Mkoani Dar es Salaam.
Ametaja changamoto nyingine ni kukosa kutambuliwa katika huduma za kijamii kama vile mifuko ya hifadhi ya jamii, huduma za bima ya afya pamoja na kukosekana kwa mikataba bora ya kazi.

Vile vile ukatili wa kijinsia kwa madereva wa kike, kukosa elimu juu ya Mambo mbalimbali yahusuyo haki na maslahi pamoja na kukosekana kwa sera zinazolinda sekta binafsi.
Amesema changamoto nyingine ni mikataba ya ukandamizaji kutoka kwa wawekezaji hasa kwa madereva wa majukwaa,
Ikiwa ni pamoja na ukosefu wa elimu na mazingira wezeshi kwa wanawake na vijana katika sekta ya usafirishaji.
” Kwa utafiti huu tunaamini utatoa mwangaza wa namna ya kutatua changamoto hizo , hasa kwa ushirikishwaji katika uundaji wa sera wezeshi na kufanikisha kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia na unyanyasaji katika maeneo ya kazi, hususan katika sekta ya usafirishaji.
” Ni imani yetu kubwa kwamba kampeni hii itaungwa mkono kusaidia uridhiaji wa mkataba Na. 190 wa ILO,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Friedrich Ebert Stiftung (FES), Christian Denzin amesema taasisi hiyo imejikita kusimamia demokrasia ya kijamii, haki na mshikamano kwa kushirikiana na COTWU – T ambacho ni sehemu ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Amesema utafiti huo uliofanywa na Michaela Collord na Nice Mwasasu unajumuisha madereva 150 wa boda boda wakiwemo wanawake 47 pamoja na mapitio ya kitaaluma, nyaraka za serikali na rupoti za sekta binafsi.