Na Mwandishi Wetu
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongella amesema baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama 2020-2024 amejiridhisha kwamba chama kinaingia katika chaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao kwa uhakika wa ushindi wa kishindo.
Akizungumza baada ya kupokea utekelezaji wa Ilani ya CCM mwaka 2020-2024 kutoka Ofisi ya Mkoa wa Shinyanga, Mongella amesema kutokana na utekelezaji mzuri wa ilani chama hicho kina uhakika wa ushindi na kwamba waendelee na kasi ya kuleta maendeleo ili kero zote ziishe.
Mongella ambaye yupo kwenye ziara ya siku saba mkoani Shinyanga kama mlezi wa mkoa huo, pia amewataka viongozi wa ngazi ya mkoa na hadi mitaa kufanya kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Mongella amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuboresha maisha ya wananchi ikiwa ni pamoja na kuleta pembejeo za kilimo kwa wakati, na maafisa ugani kutoa elimu kwa wakulima.
Awali akizungumzia kilimo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amesema kutokana na mvua nyingi za msimu wa kilimo uliopita, uzalishaji wa zao la pamba umepungua. “Kutokana na mvua nyingi, uzalishaji wa zao la pamba umepungua kwa kiasi kikubwa, lakini mazao mengine kama tumbaku na mpunga uzalishaji ni wa kuridhisha,” amesema
.Amesema kwa sasa serikali imejikita katika kuhakikisha miradi yote iliyoko kwenye ahadi za uchaguzi 2020-2025 inatekelezeka kwa wakati.
Pia, Mongella amesisitiza umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, akibainisha kuwa wao ni nguvu kazi ya taifa na wanayo nafasi kubwa ya kuchangia ustawi wa jamii.
Ameesema ni muhimu kwa vijana kujihusisha na kilimo cha kisasa na kutumia teknolojia ili kuongeza tija.
Mongella amepongeza juhudi za serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, hospitali, na shule, na kusema kuwa juhudi hizo zimeongeza imani ya wananchi kwa chama hicho.
Amesema kuwa serikali inatekeleza kwa vitendo ahadi zake na kwamba wananchi wanaona mabadiliko.
Katika sekta ya afya, Mongella amesifu serikali kwa kuboresha huduma za afya na kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya.
Amesema hatua hizi zimepunguza vifo vya akina mama na watoto na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.
Vilevile, ametoa wito kwa viongozi wa afya kuongeza juhudi katika kutoa elimu ya afya kwa wananchi.
Amepongeza jitihada za viongozi wa mkoa katika kupambana na rushwa na ufisadi, akisema kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha juhudi za maendeleo.
Mongella amesisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi waadilifu na wenye kujali maslahi ya wananchi, na kuwaasa wananchi kuwafichua wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa
.Mongella pia amezungumzia umuhimu wa mazingira na alitoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kupanda miti na kulinda vyanzo vya maji.
Amesema kuwa suala la uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja, na kwamba serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Katika ziara yake, Mongella atatemblea Shinyanga Mjini, Kahama, Msalala, Ushetu, Shinyanga Vijijini na kufanya mikutano ya ndani na hadhara.