Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa Kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, imefanya ukaguzi wa kushtukiza ili kutathmini hali ya usafiri nchini kipindi hiki cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Katika ukaguzi huo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, Habibu Suluo na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani. Ramadhani Ng’anzi waliufanya jana Disemba 21, 2024 katika Kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani cha Magufuli mkoani Dar es Salaam.
Suluo amesema Latra imefanya tathmini ya utekelezaji wa masharti ya leseni ikiwemo matumizi sahihi ya kitufe cha utambuzi wa dereva na matumizi sahihi ya tiketi mtandao.
Amesema hali ya usafiri ni salama hakuna msongamano wa abiria hali iliyochangiwa na huduma za usafiri za saa 24, huduma za usafiri wa treni ya kisasa ( SGR), zinazofanya safari Dar es Salaam hadi Dodoma,
Na Reli ya Kati zinazofanya safari za Dar hadi Arusha, zimeongeza safari mara tatu kwa juma.
Pia Mkurugenzi Mkuu huyo wa LATRA. amewataka abiria kuhakikisha wanapewa tiketi za kieletroniki na kupiga simu bila malipo namba 0800 110019 ama 0800110020 kutoa taarifa kwa mamlaka wapatapo changamoto wakiwa safarini.
Kwa upande wake Ng’anzi amewataka madereva kutii sheria bila shuruti, watakaokiuka watachukuliwa hatua kali za kisheria.