Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema hakuna sababu kwa mwananchi aliyejiajiri kushindwa kujiunga na Mfuko huo, kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika ambayo yanawawezesha wanachama wa kundi hilo kunufaika na mafao mbalimbali sawa na waajiriwa wa sekta ya umma na binafsi.
Mshomba ametoa kauli hiyo wakati alipowaongoza wafanyakazi wa NSSF kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kuandikisha wanachama wapya katika soko la Tegeta Nyuki jijini Dar es Salaam, kupitia kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi.
Amesema mwananchi aliyejiajiri atakapojiunga na NSSF atanufaika na mafao mbalimbali yakiwemo pensheni ya uzeeni, urithi, ulemavu, uzazi, matibabu pamoja na mafao mengine ambayo awali hayakupatikana kwa kundi hilo.
“Tunaposema wanachama wa NSSF ni mastaa wa mchezo, tunamaanisha kuwa Mfuko unatoa uhakika wa maisha bora, huduma za matibabu na kipato hata baada ya mwanachama kustaafu.

“Endapo mwanachama atafariki, wategemezi wake watanufaika na mafao ya urithi,” amesema.
Aliongeza kuwa NSSF imeboresha mfumo wa uchangiaji kwa kuufanya kuwa rahisi na rafiki kwa wananchi.
Amefafanua kuwa mwananchi anayechangia Sh. 30,000 kwa mwezi atanufaika na mafao yote ikiwemo matibabu, huku anayechangia Sh. 52,200 kwa mwezi atanufaika yeye, mwenza wake pamoja na wategemezi wasiozidi wanne.
Mshomba ameeleza kuwa uchangiaji si lazima ufanyike kwa mkupuo mmoja, bali unaweza kufanyika kwa utaratibu wa kila siku, wiki, mwezi au msimu, kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali bila ulazima wa mwananchi kufika ofisi za NSSF.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Omary Mziya, amewahamasisha wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Naye Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, Lulu Mengele, amesema kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi itaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa soko hilo, Katibu wa Soko la Tegeta Nyuki, Omary Hemed, ameishukuru NSSF kwa kuendelea kuwafikia wananchi sokoni hapo kwa kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kuwapa fursa ya kujiunga na kuchangia, hatua ambayo imewawezesha wengi kunufaika na mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu.

























