Na Mwandishi Wetu
MWANZA: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amekabidhi tuzo kwa waajiri wanaowasilisha kwa wakati michango ya wafanyakazi wao katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ikiwa ni sehemu ya kutambua uadilifu na uwajibikaji wao katika kulinda haki za wafanyakazi.
Mkenda amekabidhi tuzo hizo katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanawake Wamiliki wa Shule na Vyuo vya Kati Tanzania (TAWOSCO), ambapo NSSF pia ilitoa elimu kuhusu hifadhi ya jamii na maboresho ya huduma mbalimbali, hasa katika matumizi ya mifumo ya kidijitali.

Kwenye mkutano huo, Mkenda ametoa pongezi kwa TAWOSCO kwa mchango wao kwenye maendeleo ya elimu nchini, huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta hiyo, hasa uboreshaji wa miundombinu na upanuzi wa fursa za elimu.
“Tunatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi, hususan wanawake wamiliki wa shule, katika kutoa ajira na kukuza elimu.
“Kwa kutambua hilo, leo tunatambua pia waajiri waaminifu wanaotekeleza wajibu wao kwa wafanyakazi kupitia NSSF,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Saidi Mtanda amewapongeza wanawake wa TAWOSCO kwa juhudi zao katika kutoa elimu, akisisitiza kuwa mchango wao ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, Meneja wa Uandikishaji, Ukaguzi na Matekelezo, Cosmas Sasi amesema hadi sasa, wanachama 131 wa TAWOSCO sawa na asilimia 66 wamejiunga rasmi na NSSF, na kati yao, wanachama 35 wanatekeleza kikamilifu wajibu wa kuchangia michango kila mwezi.
Amesisitiza kuwa kuna haja kwa wanachama wenye malimbikizo kuwasiliana mapema na ofisi za NSSF ili kuweka mipango ya ulipaji, badala ya kusubiri hatua za kisheria ambazo zinaweza kuepukika kwa mawasiliano ya karibu.

Akizungumzia maboresho ya huduma, Sasi ameeleza kuwa NSSF imeongeza ufanisi kwa kuanzisha mifumo ya kidijitali ikiwemo NSSF Portal, NSSF App, WhatsApp Chatbot, pamoja na huduma za USSD na SMS, zinazowawezesha wanachama na waajiri kupata huduma nyingi bila kufika ofisini.
Katika risala yao, Makamu Mwenyekiti wa TAWOSCO, Christa Rweyemamu ameeleza kuwa umoja huo una wanachama 195 wanaohudumia zaidi ya wanafunzi 900,000 na kutoa ajira kwa zaidi ya watu 5,000 nchini.

Ametoa shukrani kwa NSSF kwa kushiriki na kusaidia kuwajengea uwezo wanachama kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii.
