Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatarajia kusaini mikataba yenye thamani ya Sh.bilioni 50.98 kwa ajili ya kuhamasisha umma kuachana na matumizi ya nishati za kupikia zisizo salama.
Ihamasishaji huo ni hatua ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi za Kupikia.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu kutoka REA) Advera Mwijage amesema hayo katika mkutano na Waandishi wa Habari Septemba 11, 2024 Jijini Dodoma.
Amesema utekelezaji wa miradi ya Nishati Safi na zilizoboreshwa za kupikia ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi 2024- 2034 ambao unaelekeza ifikapo Mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi za kupikia.
“Hivi karibuni, Wakala utasaini mikataba kadhaa ya ushirikiano na wadau mbalimbali ambayo yote kwa pamoja imelenga kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi za Kupikia kwa wote kama Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati safi za Kupikia unavyoelekeza,,” amesema.
Amesema kwa upande wa Jeshi la Magereza, mikataba itakayosainiwa ina thamani ya sh bilioni 35.23 ambapo kati ya fedha hizo asilimia 75.5 ambayo ni sawa na shi bilioni 26.57 zitatolewa na REA na asilimia 24.6 sawa na sh bilioni 8.66 zitatolewa na Jeshi la Magereza kwa Mradi utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika Magereza 129 yaliyopo Tanzania Bara.
“Katika mkataba huu na Magereza kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa mifumo ya bayogesi 126, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG, usimikaji wa mfumo wa gesi asilia,
“Pia usambazaji wa mitungi ya gesi (LPG) ya kilo 15 ikiwa na jiko la sahani mbili ipatayo 15,920 kwa watumishi wa Magereza, usambazaji wa tani 865 za mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kutoka STAMICO,” amesema.
Amesema mkataba huo wa Magereza utahusisha pia usambazaji wa mashine 61 za kutengeneza mkaa mbadala, ujengaji uwezo kwa watumishi 280 wa Jeshi la Magereza na usambazaji wa majiko banifu 977.
Kati ya majiko hayo, 377 yatatumia nishati ya bayogesi, 256 yatatumia LPG na 344 yatatumia nishati ya mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kwa kuanzia na baadaye kwa mkaa unaotokana na mabaki ya mazao mbalimbali.
Kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), amesema mikataba itakayosainiwa ina thamani ya sh. bilioni 5.75 ambapo kati ya fedha hizo asilimua 76 ambayo ni sawa na sh. bilioni 4.36 itatolewa na REA na huku asilimia 24 sawa na sh. bilioni 1.39 itatolewa na JKT.
Amesema katika kuwezesha kaya za vijijini na zile zilizopo katika maeneo ya vijiji-miji kutumia nishati safi za kupikia na zilizoboreshwa, Serikali kupitia REA inaendelea kutoa ruzuku katika uuzaji wa wa mitungi ya gesi (LPG) ya Kilo 6.
Ametaja kampuni zilizoshinda zabuni ya kusambaza mitungi hiyo kuwa ni Taifa Gas, Manjis, Oryx pamoja na Lake Oil ambapo alisema mitungi 452,445 itasambazwa kwa bei ya ruzuku katika mikoa yote ya Tanzania Bara na huku kila wilaya ikinufaika na mitungi 3,255.