Na Mwandishi Wetu
TUNDUMA: MGOMBEA urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu ametaja hatua mbalimbali ambazo chama chake kitaweka mbele iwapo kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kwa lengo la kunusuru sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Tunduma, mgombea huyo amesema moja ya hatua ni kufungamanisha kilimo na viwanda ili kuhakikisha kuwa mazao ya wakulima yanapata soko la uhakika na kuongeza thamani ya mazao hayo kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.

Ameeleza pia kuwa serikali yao itaacha kuuza malighafi za kilimo na badala yake kuweka mkazo katika usindikaji wa bidhaa hizo ndani ya nchi.
Kadhalika, ameeleza kuwa serikali yake itaongeza ukubwa wa eneo la kilimo hadi kufikia ekari milioni tatu hadi tano, kwa lengo la kuongeza uzalishaji kwa matumizi ya ndani na viwandani.
Katika kuboresha mazingira ya uzalishaji, mgombea huyo ameahidi kuongeza bajeti ya kilimo kutoka asilimia nne ya sasa hadi kufikia kati ya asilimia saba hadi nane ndani ya miaka mitano, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuipa sekta hiyo uzito unaostahili katika ajenda ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza kuhusu mfumo wa masoko ya mazao, ameahidi kuweka uhuru wa soko kwa kufuta utaratibu wa stakabadhi ghalani na mfumo wa kilimo cha mkataba kupitia vyama vya ushirika kama Chama cha Ushirika wa Masoko ya Mazao ya Kilimo (AMCOS), hatua ambayo inalenga kumuwezesha mkulima kupata faida stahiki kutokana na jasho lake.
Hatua nyingine alizozitaja ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kilimo itakayoshughulikia masoko, utafiti, mahitaji ya kiufundi katika kilimo pamoja na kusimamia hifadhi ya taifa ya chakula.
Amesema mamlaka hiyo itakuwa nguzo muhimu katika kupanga na kuratibu maendeleo ya sekta hiyo kwa njia ya kisasa na endelevu.
Aidha, amesema serikali yake itaweka mkazo katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara, umwagiliaji na ujenzi wa maghala kwenye maeneo ya kilimo makubwa kama vile Mabonde ya Magugu, Bahi, Igunga, Tanganyika, Bonde la Kilombero, Ziwa Rukwa na Kyela, ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa mazao.
Vilevile, ameahidi kuanzisha Mfuko wa Kudhibiti Bei utakaosaidia kukabiliana na mabadiliko ya bei ya mazao sokoni, pamoja na kuanzisha na kuimarisha vyuo vya kilimo nchini ili kuongeza ujuzi na maarifa kwa wakulima na wataalamu wa sekta hiyo.
Kwa mujibu wa mgombea huyo, hatua hizo zinalenga kuifanya sekta ya kilimo kuwa na tija, endelevu, na yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.