MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Sauti Ya Umma (SAU), Majalio Kyara amesema akichaguliwa kushika wadhifa huo ataongoza nchi kwa hofu ya Mungu akitengeneza Taifa na watumishi wenye hofu ya Mungu.
Amesema hayo Dar es Salaam katika uzinduzi wa kampeni ya chama hicho kwa ajili ya kugombea nafasi ya Urais, Wabunge na Madiwani katika uchaguzi mkuu unaotarajiw akufanyika Oktoba 29,2025.
Amesema viongozi wanahitajika kuongoza taifa kupitia misingi ya wazee yenye kuondoa misingi iliyopotea,ikiwemo maadili uadilifu , ili kuwa na upendo, uwajibikaji, uadilifu, haki na bila dhuluma ili kutengeneza taifa lenye hofu ya Mungu.

Kuhusu uchaguzi amesema SAU inaongozwa na ilani yenye nguzo tatu, ikiwemo kilimo, viwanda na teknolojia.
“Kilimo ni kama damu kwenye mwili wa binadamu, kilimo kipewe umuhimu, kwani kupitia kilimo tunatatua changamoto nyingi kwenye taifa ikiwemo afya, ajira na uchumi,” amesema Kyara.
Amesema SAU inahamasisha kilimo hai ili wananchi wa Tanzania wapate chakula kilicho bora, ambapo wataondoa matatizo mengi ya kiafya.

“Upo umuhimu mkubwa wa kupambana na afya kupitia kwenye kilimo kwa kuangalia kilimo hai na kurejesha mbegu za asili,” amesema na kuongeza kuwa afya ya mtanzania ni jambo la kupigania kwa nguvu zote.
Aidha amesema ipo haja ya kufungua fursa za kiuchumi Tanzania, kwa kuwa kuna mkwamo mkubwa,kukihitajika wawekezaji wazawa.

Amesema akichaguliwa kuingia madarakani atatengeneza mifumo ambayo uchumi wa Tanzania unashikwa na wazawa.
Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama hicho, Safia Mussa amesema chama hicho kinajikita kuimarisha viwanda, kilimo na teknolojia, wakitaka wakulima kupata pembejeo.
Amesema wakichaguliwa hawatowadanya wananchi bali watakuwa nao bega kwa bega ili wajue matatizo yao.