Na Mwandishi Wetu, Busega
SIMIYU:MFANYABIASHARA wa Mji mdogo wa Lamadi ambaye pia ni mdau wa Maendeleo, Joseph Goryo ameshinda tuzo ya kuwa mlipa kodi Bora wa Wilaya ya Busega katika sherehe zilizofanyika Mjini Bariadi.
Katika tukio hilo, utoaji wa Tuzo za Mlipa kodi bora kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo walipa kodi kuanzia ngazi ya Chini, kati na Juu wote walitambuliwa na kupewa tuzo kwa kuwa walipa kodi hodari bila kukwepa.
Goryo ni mdau anayesaidia watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo pia kusomesha watoto wa kike wale waliotoka katika mazingira magumu.
Tuzo hiyo amekabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faidha Salim tukio lililowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Wafanyabiashara na viongozi wa Serikali na sekta binafsi.
Tuzo hizo za mlipa Kodi Bora zinatolewa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) zikitolewa nchini kote kila mwaka kwa wafanyabiashara vinara katika ulipaji Kodi nchini.