Na Mwandishi Wetu
KIBAHA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ameipongeza Shule ya Sekondari Kibaha kwa kuwa miongoni mwa shule bora nchini kwa matokeo ya mitihani ya kitaifa, huku akitoa wito kwa walimu na uongozi wa shule hiyo kuhakikisha kiwango cha ufaulu hakishuki.
Mchengerwa ametoa pongezuli hizo akiwa kwenye ziara, ambapo alikagua miundombinu ya shule hiyo ikiwemo madarasa, mabweni, maabara, na maeneo ya wanafunzi wa bweni, kabla ya kuzungumza na walimu pamoja na wanafunzi waliokuwa wakijiandaa kuanza kidato cha tano.

“Nawapongeza sana kwa matokeo mazuri ambayo yanaifanya Kibaha kuwa alama ya ubora wa elimu nchini. Hata hivyo, changamoto ya sasa ni kuhakikisha mnaendelea kushikilia kiwango hiki au kupanda zaidi licha ya ongezeko la wanafunzi,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Jimmy Nkwamu amesema ufaulu wa mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka huu umefikia asilimia 93.7, ambapo wanafunzi 136 kati ya 140 walipata daraja la kwanza.
Aidha, kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2024, asilimia 52 ya wanafunzi walipata daraja la kwanza, huku hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la tatu, la nne, au la sifuri.

Mchengerwa ameridhishwa na juhudi za walimu na uongozi wa shule hiyo, akisisitiza kuwa Kibaha Sekondari ni mfano wa kuigwa katika sekta ya elimu.
Amesema ni muhimu kwa shule hiyo kuwa na mikakati madhubuti ya kitaaluma na kitaasisi ili kuhakikisha kuwa ubora unaendelea kuimarika licha ya changamoto ya ongezeko la wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu.
“Nataka kuona mikakati ya kudhibiti changamoto zitokanazo na idadi kubwa ya wanafunzi. Walimu mnatakiwa kuwa wabunifu zaidi ili kutobadili mwelekeo huu mzuri,” amesema.

Kwa upande mwingine Waziri Mchengerwa ametoa agizo kwa Ofisa Elimu wa Mkoa kufanya ziara katika wilaya zote za Mkoa wa Pwani ili kubaini changamoto za kielimu na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.
“Nakuagiza ufanye ziara katika kila wilaya ya mkoa huu na kuhakikisha changamoto zote za kielimu zinaainishwa na kutafutiwa suluhisho. Hatutaki kuona maeneo ambayo yanazorota kimatokeo wakati wengine wanapaa,” amesema.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha sekta ya elimu kwa kuhakikisha uboreshaji wa miundombinu, mazingira ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuongeza uwajibikaji kwa watendaji wa elimu katika ngazi zote.