Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Ngorongoro, Yanick Ndoinyo, amesema jimbo hilo ni la kimkakati kwa kuwa ni eneo maarufu kwa utalii, ufugaji na kilimo, hivyo anatambua kuwa ana majukumu mazito ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Akizungumza na wanahabari katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Ndoinyo amesema amejipanga kuhakikisha changamoto zilizopo wilayani zinabadilishwa kuwa fursa za maendeleo.
Amesema Kipaumbele chake cha awali ni kubadilisha taswira ya wilaya na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya serikali na wananchi, ili mipango ya maendeleo ipokelewe kwa urahisi na kwa maelewano makubwa.
Ameeleza kuwa, kwa bahati mbaya, wilaya ya Ngorongoro ipo pembezoni na makao makuu yake bado yanaonekana ya kijijini,lengo ni kujenga barabara ya lami inayounganisha wilaya hiyo na mkoa wa Arusha, pamoja na kuifanya kuwa kivutio kikubwa cha utalii.
Kwa sasa, fursa za utalii zinatekelezwa kwa takribani asilimia 50, hivyo dhamira ni kuzitekeleza kwa asilimia 100.
Aidha, amesema sekta ya ufugaji inapaswa kubadilishwa na kuendeshwa kibiashara zaidi, badala ya kutegemea mila kama ilivyo sasa.
Pia, ni ndoto yake kuhakikisha wilaya inapata mfuko wa kutunisha mitaji utakaowawezesha wananchi kujiajiri na kuongeza kipato chao.
Ndoinyo amesisitiza kuwa mikakati yote hiyo itafanikiwa endapo kutakuwepo na ushirikiano mzuri kati ya wananchi na serikali yao. Lengo kuu ni kuhakikisha serikali, wilaya, wananchi na taifa wanazungumza lugha moja kuhusu maendeleo ya Ngorongoro.
Ameongeza kuwa ni muhimu Watanzania waendelee kuwa na imani na Bunge la 13, ambalo linafahamu changamoto za wananchi na lina wabunge wengi wa CCM wanaotekeleza Ilani ya chama kwa ufanisi.
Katika awamu yake ya kwanza, Ndoinyo amesema atatumia mahusiano na uzoefu wake wa kimataifa kutekeleza miradi mbalimbali, kuboresha taswira ya Bunge kwa wananchi, na kuongeza imani yao kwa chombo hicho cha uwakilishi.

