Na Lucy Lyatuu
TAASISI ya Mwalimu Nyerere (MNF) imesema matukio yaliyozuka nchini ya kulawiti,kuteka,kunyanyasa na kuua wengine ni ya aibu na kwamba wenye madaraka kikatiba kuhudumia wananchi wawajibike bila uoga.
Imesema baada ya tamko la Rais Samia Suluhu Hassan la kuagiza wenye mamlaka kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na mauaji na kuchunguza tukio hilo ,MNF ilitegemea wawepo wenye kupeleka barua za kuachia madaraka.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MNF, Joseph Butiku amesema hayo leo Dar es Salaam wakati Taasisi hiyo ikitoa taarifa kuhusu tabia mbaya zinazohatarisha Usalama wa maisha ya Watanzania na mali zao.
Amesema Kwa tabia hizo mbaya zilizozuka ni Kwa Nini Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na hata Mkuu wa Jeshi la Ulinzi (CDF) wasichukue hatua?
” Tatizo la utekaji halijaanza Leo, wakati wa Mwalimu Nyerere yalikuwepo Ila aliwawajibisha na Kwa sasa jambo la kuwajibika ni kama linafifia,” amesema Butiku na kuongeza kuwa kama kiongozi umepewa kazi ni kuwajibika na sio kusema Rais ameagiza uchunguzi ufanyike.
Amesema kipindi Cha Mwalimu Nyerere aliyekuwa Rais wa Awamu ya pili,Hayati Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwajibika na hata Natepa aliwajibika wakati wa uongozi wake.
Amesema sio kusema kuwa wahalifu hawajulikani kwani wanajulikana Kwa kuwa wanaishi miongoni mwa jamii katika kaya, wako ndani ya vyombo vya dola,wako makanisani na katika misikiti.
“Tunawajua lazima serikali yetu iwajue, hivyo Taasisi ya MNF inaomba tumsaidie Rais kupata taarifa sahihi kuhusu wabaya hao ili achukue hatua stahili,anavyo vyombo vya dola vyenye majukumu- mahsusi ya kumpa taarifa za uhakika,” amesema na kuongeza kuwa haiwezekaniki kuwa na miaka 62 ya uhuru bila kuwajua waahalifu nchini.
Amesema wenye madaraka hayo waliyopewa na Rais Samia waonekane waziwazi wakiwajibika na sio kunyoosheana vidole na pia Taifa halihitaji IGP na CDF kusema hawajui kwani ni lazima kujua.
Amesema Rais ni mmoja tu sio wawili wala watatu waliokabidhiwa Katiba ya nchi ili kuitumia kuongoza Taifa na kulinda na kuhakikisha usalama wa Watanzania wote na wageni halali wanaoingia katika Taifa na pia kulinda mali za Watanzania.
Amesema huo ni wajibu wa Kikatiba wa Rais na kwamba anautekeleza kwa niaba ya Watanzania hivyo aungwe mkono bila maswali.
Butiku amesema Taifa la Tanzania sio la wauaji wala la wahuni, ni Taifa la watu wanaoishi kwa kuzingatia Katiba ya nchi na sheria zinazotokana na Katiba hiyo hivyo ni wajibu wa kufuata na kutii Katiba na sheria zote zinazotokana Katiba hiyo, na ambazo hazikiuki Katiba.
“Hakuna nafasi wala ruhusa kwa raia yoyote wa nchi hii kuishi nje ya utaratibu huu. Huu ndio msingi wa amani, umoja, na maendeleo yanayo shirikisha wananchi wote kwa faida yao. Kwa maana hii, sisi Watanzania ni wastaarabu.,” amesema.