Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewapatia waandishi wa habari wa mtandaoni nafasi kubwa ya kushiriki katika shughuli za kitaifa, tofauti na ilivyokuwa awali.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari wa Kimtandao Tanzania (JUMIKITA), Shaabani Matwebe, amesema hayo wakati akizungumza katika kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na Star TV.
Matwebe amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa nafasi kwa JUMIKITA kwa kuwawezesha kushiriki katika matukio muhimu ya kitaifa, ikiwemo misafara ya viongozi wakuu wa serikali.
“Katika kitu ambacho niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita ni kwamba sisi baada ya kuunda jumuiya na kutafuta njia mbalimbali za kushirikiana na serikali, tumepokelewa vizuri.
“Waandishi wa habari wa mtandaoni sasa wanashiriki katika misafara mikubwa ya viongozi, jambo ambalo zamani halikuwepo,” amesema.
Ameongeza kuwa, awali kabla ya kuanzishwa jumuiya hiyo 2021,
waandishi wa habari wa mtandaoni walikumbwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kutotambuliwa rasmi na taasisi za serikali.
Amesema jitihada kubwa zimefanyika hivi sasa waandishi wa habari za mitandaoni wanatambuliwa katika sekta ya habari.
Kwamba kuoitia JUMIKITA, waandishi wengi wa habari wa mtandaoni wamepata mafunzo ya maadili ya uandishi wa habari, wengine wakipata fursa ya kushirikiana na taasisi za serikali na sekta binafsi.
Ameagiza wanajumuiya hiyo kuzingatia weledi na maadili katika kazi wanazozifanya.
“Sera za serikali ni nzuri, na toka Awamu ya Sita imeingia madarakani, tumeweza kufanya kazi kwa uhuru zaidi.
“Hata hivyo, waandishi wa habari wa mitandaoni wanapaswa kuwa makini, kufuata maadili na kuhakikisha wanatoa habari sahihi na zenye ukweli,” amesema.
JUMIKITA inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhakikisha waandishi wa habari wa mtandaoni wanapata mazingira bora ya kazi, fursa za mafunzo na ulinzi wa haki zao.