FEBRUARI 4, 2024:KIFO cha Ole Mushi chaibua, wanajamii, wanasiasa nchini
Thadei Ole Mushi aliyeiteka mitandao ya kijamii kwa uchambuzi na uchangiaji wa mada mbalimbali hususan za kisiasa, amefariki dunia.
Kifo chake kimewagusa wanasiasa na wana jamii kutokana na umaarufu wake katika kuchambua mada mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii.
Ole Mushi ambaye ni kada wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), amefariki dunia Februari nne, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ( JKCI), jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.
FEBRUARI 10, 2024: LOWASSA 1953-2024 mwamba umelala
WAZIRI Mkuu mstaafu wa Tanzania Edward Lowassa amefariki dunia, akiwa anapatiwa matibabu jijini Dar es Salaam.
Tangazo la kifo cha Lowassa kimetangazwa Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika tangazo fupi alilolitoa kupitia televisheni ya Taifa, Mpango amesema kuwa Lowassa amefikwa na umauti katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ( JKCI), jijini Dar es Salaam.
”Amefariki leo akipatiwa matibabu kwa ugonjwa wa kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu. Hayati Ngoiyai Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu tangu Januari 14, 2022”.
FEBRUARI 29, 2024: 1925 -2024 Rais Ali Hassan Mwinyi amefariki dunia
RAIS wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amefariki dunia leo, Alhamis Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Nzena jijini Dar es Salaam, alikokuwa akioatiwa matibabu.
MACHI 23,2024 Sabodo afariki
BILIONEA maarufu nchini, Mustafa Jaffer Sabodo amefariki Dunia leo alfajiri akiwa nyumbani kwake, Masaki jijini Dar es Salaam, mtoto wa marehemu, Danstan amethibitisha.
“Mzee amefariki leo alfajiri akiwa nyumbani. Taratibu za mazishi zinaendelea na atazikwa katika makaburi yaliyoko mtaa wa Bibi Titi Mohamedi karibu na CBE,” amesema Danstan.
Marehemu Sabado alizaliwa mkoani Lindi na alikuwa akifanya biashara katika nchi za Ufaransa, India, Kenya, Sudan, Nigeria, Zimbabwe na Tanzania.
OKTOBA 29, 2024 Buriani Jenerali David Masuguri
Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali David Bugozi Musuguri, amefariki dunia Oktoba 29, 2024 akiwa na umri wa miaka 104, akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo jijini Mwanza.
Jenerali Musuguri, alizaliwa Januari 4, 1920, Butiama mkoani Mara.
Pia alihudumu katika jeshi kutoka 1942 hadi 1988 na kuhitimisha uongozi wake kama Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kutoka 1980 hadi 1988.
NOVEMBA 9, 2024 Lawrence Mafuru afariki, Samia, viongozi wamlilia
Aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru amefariki dunia leo Jumamosi Novemba 9, 2024 katika Hospitali ya Apollo nchini India.
Rais Samia Suluhu Hassan ameomboleza kifo cha mafuru akitoa pole kwa familia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji).
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Lawrence Nyasebwa Mafuru, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kilichotokea leo Novemba 9, 2024 katika hospitali ya Apollo nchini India.
NOVEMBA 27, 2024: Ndungulile afariki dunia kabla ya kukalia kiti chake WHO
MBUNGE wa Kigamboni ambaye pia ni Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt Faustine Ndugulile, amefariki dunia India alikokuwa anapatiwa matibabu.
DISEMBA 17,2024: Tendwa afariki Msajili wa Zamani Vyama vya Siasa
Aliyewahi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Bill Tendwa amefariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema marehemu Tendwa amefariki leo Desemba 17, 2024 katika Hospitali yall Taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.
DISEMBA 22, 2024: Mkurugenzi Ofisi ya Msajili wa hazina, bintiye wafariki ajalini Same
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko amefariki dunia.
Nnko amefariki katika ajali ya gari iliyotokea Same Kilimanjaro, Disemba 22, 2024.
Katika ajali hiyo pia binti yake wa kwanza Maureen amefariki dunia.
Imeandaliwa na Lucy Ngowi