Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema matokeo ya usaili wa maandishi kwa watahiniwa walioomba nafasi za kazi katika Mamlaka hiyo, yatatangazwa Aprili 25 mwaka huu.
Imesema matokeo hayo ya usaili uliofanyika Machi 29 na 30 mwaka 2025 yatatangazwa kupitia Tovuti ya TRA (www.tra.go.tz) baada ya kuwasilishwa na Mshauri elekezi Aprili 23, mwaka huu.
Akizungumzia mchakato huo wa ajira za TRA Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali watu na Utawala Moshi Jonathan Kabengwe amesema baada ya majina kutangazwa Mei 2 hadi 4 utafanyika usaili wa Vitendo kwa Madereva na Waandishi Waendesha Ofisi.
Amesema baada ya Usaili wa Vitendo utafuata Usaili wa mahojiano kwa kada nyingine ambao utafanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 7 hadi 9 2025 ambapo watakaofanikiwa kushinda Usaili huo wataarifiwa Mei 18,.2025 na kuanza mafunzo Elekezi Mei 22,2025 mpaka Juni 02,2025 watakapoajiriwa na kuanza kazi rasmi.
Kabengwe ameeleza kuwa katika mchakato wa usaili maombi yaliyokidhi vigezo yalikuwa 112,952 yakaongezeka maombi 71 baada ya kukata Rufaa na kufikisha idadi ya maombi 113,023 yaliyohusisha waombaji 86,314 na waliofanya Usaili wa maandishi ni waombaji 78,544 sawa na asilimia 91 ya waombaji wote na waombaji 7,770 sawa na asilimia tisa hawakufika kwenye Usaili kwa sababu mbalimbali.
Ameeleza kuwa Sera ya TRA ni ajira sawa kwa wote na ajira zilizotangazwa zitazingatia sifa na vigezo vya muomba kazi bila kujali hali ya muhusika kwamba ni Mtoto wa Maskini, Mtoto wa Kiongozi au Mtoto wa Mtumishi wa Umma ndiyo maana vituo vya Usaili viliwekwa kwenye mikoa nane na Zanzibar ili kusogeza huduma karibu.
Aidha Kabengwe ameshukuru kuwepo kwa mrejesho kutoka kwa Jamii kupitia njia mbalimbali na kueleza kuwa kama yupo mwenye Taarifa zinazoashiria kuharibu zoezi la ajira awasiliane na TRA kupitia Sikika App, namba za Simu Bure 0800 750 075 / 0800 780 078 / 0800 110 016 au Whatsapp 0744 233 333 au E-mail huduma@tra.go.tz / services@tra.go.tz au atoe Taarifa TAKUKURU