Na Lucy Lyatuu
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt Moses Kusiluka amewataka Maofisa Habari wa Serikali kukujipanga kiteknolojia wakizingatia weledi, maadili na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha mawasiliano ya serikali na wananchi pamoja na kulinda maslahi ya Taifa katika mazingira ya kasi kubwa ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Amesema bado hawako vizuri katika matumizi ya teknojia ya Habari na mawasiliano katika kuwaunganisha wananchi na serikali kwa kutoa ufafanuzi wa haraka na taarifa hata kwa wale wanaoshambualia nchi kwa njia ya uanaharakati.
Akizungumza katika kikao kazi cha Maofisa hao leo Dar es Salaam alisema serikali inawategemea wataalamu hao kama kundi muhimu katika kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa ufasaha, hususan katika kipindi ambacho teknolojia imetumika vibaya kwa kutoa taarifa potofu na propaganda zenye kuhatarisha usalama na mshikamano wa nchi.
Katibu Mkuu Kiongozi alisema teknolojia ya habari imeleta fursa kubwa lakini pia changamoto, akionya kuwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali yanaweza kuleta madhara makubwa endapo hayatadhibitiwa kwa weledi na uzalendo.
“Tumeshuhudia teknolojia ilivyotumika vibaya na maadui kushambulia nchi yetu, tumekuja hapa tujiulize ninyi maofisa Habari mko wapi, mlikuwa wapi,” alihoji Katibu Mkuu na kuongeza kuwa bado hawajachelewa kwa kuwa Tanzania inayotakiuwa inajengwa na wenyewe na maofisa Habari watambue kuwa wanategemewa.
Aliwakumbusha kuwa wao ni watumishi wa umma walioajiriwa na hivyo wanapaswa kutambua nafasi walizonazo ni dhamana na bahati kubwa inayopaswa kulindwa kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Katibu Mkuu Kiongozi alisisitiza kuwa jukumu la Ofisa Habari si kumsifu au kumfurahisha kiongozi, bali ni kutoa taarifa sahihi za kazi, mipango na mafanikio ya serikali, Pamoja na kukusanya kero za wananchi na kuzifikisha kwa wahusika ili zipatiwe ufumbuzi.
Alieleza kuwa bado serikali haijafanya vizuri vya kutosha katika kuwafikia wananchi kwa taarifa sahihi kuhusu miradi na mipango mikubwa ya maendeleo, hali inayosababisha wananchi kukosa uelewa wa fursa zilizopo na mchango wa serikali katika kuboresha maisha yao.

Dkt Kusiluka aliwataka Maofisa hao kujifunza kwa kina nyaraka muhimu za taifa ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025, akisema humo ndimo kunakopatikana mwelekeo wa sera, miradi na ahadi zinazotekelezwa na serikali, hivyo ni chanzo muhimu cha taarifa kwa wananchi.
Aidha, alihimiza mshikamano na ushirikiano baina ya Maafisa Habari wa taasisi mbalimbali za serikali, akisema serikali ni moja na inapaswa kuwasiliana kwa sauti moja, badala ya kila taasisi kufanya kazi kivyake kama kisiwa.
Alibainisha pia umuhimu wa kuwa washauri wa kimkakati wa viongozi wao katika masuala ya mawasiliano, kwa kuwa wao ndio wataalamu waliobobea katika tasnia hiyo, hivyo wanapaswa kusimama imara katika kutoa ushauri wa kitaalamu bila woga.
Kadhalika alihimiza kujiendeleza kitaaluma kwa kujifunza mbinu za kisasa za mawasiliano, kushirikiana na sekta binafsi na kuachana na mtazamo wa kuridhika au kusimama katika maarifa ya zamani.
Balozi Kusiluka alisema maofisa hao wa Serikali wako mstari wa mbele katika kujenga umoja wa kitaifa, kulinda amani na kutetea maslahi ya nchi, hivyo wanapaswa kutumia taaluma yao kikamilifu kuhakikisha serikali inawafikia wananchi na dunia kwa ufanisi, uwazi na uaminifu.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema maofisa Habari wa serikali 500 kati ya 800 kutoka serikali kuu na serikali za mitaa wamekusanyika kwa siku mbili ili kupeana miongozo na maelekezo mbalimbali.
Mshauri wa Rais Masuala ya Habari, Tido Mhando alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ana maono ya kuleta ammabo mazuri kwa masuala ya Habari na kwamba lengo ni Habari zitolewazo ziwe sahihi na ziguse kila mahali.
Alisema matarajio ni kutoa taarifa sahihi zenye kueleza uelekeo mzuri na sura nzuri ya taifa.

