Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu wa Kassim Majaliwa, amesema elimu ya watu wazima ni zaidi ya masomo ya kawaida, pia zana muhimu ya kuleta maendeleo endelevu kwa taifa.
Akizungumza leo Agosti 25, mwaka 2025 alipofungua kongamano la kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Majaliwa amesema elimu hiyo ina mchango mkubwa katika kuongeza kipato, kuboresha ustawi wa kijamii, afya na ushiriki wa kiraia.

“Elimu si tukio la muda, bali ni safari endelevu ya kujifunza katika maisha yote. Elimu ya watu wazima haimuhusu mtu mzima pekee, hata vijana wanaweza kujiunga na kunufaika na programu mbalimbali za ujuzi zinazotolewa na taasisi hii,” amesema Majaliwa.
Ameongeza kuwa uzoefu wa kimataifa unaonesha kuwa elimu ya watu wazima ni chombo muhimu katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na binafsi.
Ameipongeza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kwa mchango mkubwa katika kipindi cha nusu karne, hususan katika kutoa elimu nje ya mfumo rasmi na kuwafikia Watanzania waliokuwa hawajapata fursa ya elimu ya msingi.

“Taasisi hii imekuwa mshauri wa Serikali katika masuala ya kisera na kitaalamu. Imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuwafikia makundi yaliyosahaulika kwa muda mrefu,” ameongeza.
Ameielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na taasisi hiyo kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watu wazima, hasa katika maeneo ya pembezoni na yenye changamoto za kijamii na kijiografia.
Vilevile, ameagiza taasisi hiyo kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya tafiti za mara kwa mara ili kubaini changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuandaa suluhisho bunifu linalokidhi mahitaji ya jamii.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
“Kupitia SEQUIP, wasichana 13,272 waliokuwa wameacha shule wameweza kurejea katika mfumo wa elimu ndani ya kipindi cha miaka mitano,” amesema.
Ameongeza kuwa mradi mwingine wa Mpango Jumuishi kwa Vijana Walioko Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu (IPOSA), umefanikiwa kuwajengea uwezo vijana 10,000 walioko nje ya mfumo rasmi katika maeneo ya stadi za maisha, ujasiriamali na ufundi wa awali.
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Profesa Philipo Sanga, amesema taasisi yake inajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya Serikali hususan katika maboresho ya sera ya elimu jumuishi inayolenga kuwafikia Watanzania wote bila ubaguzi.
“Sera hii ya elimu jumuishi imekuwa chachu ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kujifunza, bila kujali umri, jinsia au hali ya maisha,” amesema.