Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini watoe mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.
Majaliwa ametoa wito huo leo Jumanne Machi 18, 2025 katika Maadhimisho ya miaka 30 ya Uanzishwaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Amesema, ” Mahitaji ya soko la ajira tutayajua kwa kufanya tafiti za mara kwa mara kwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa,”.

Amesema katika zama hizi zenye kasi ya maendeleo ya teknolojia, ni muhimu kwa VETA kuendelea kujiimarisha kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
“Toeni mafunzo ya ufundi stadi yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia, mafunzo hayo yajumuishe ujuzi wa teknolojia za kisasa zinazochochea uzalishaji wenye tija,” amesema.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa Elimu ya Ufundi Stadi, Majaliwa amesema kuwa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinaonesha kuwa takribani asilimia 70 ya ajira zote ni ajira binafsi na kwa watu wenye elimu ya ufundi stadi hasa kwenye sekta za kilimo, ujenzi, usafirishaji, na huduma za kijamii.

“Kwa upande wa nchi yetu, takwimu za ajira zilizozalishwa kati ya mwaka 2020 na 2024 zinafikia Milioni saba ambapo ajira binafsi katika sekta isiyo rasmi imeajiri watu milioni 6.1 sawa na asilimia 87.1 ambapo wengi wao wana elimu ya ufundi stadi, na sekta rasmi imeajiri watu 907,873 ambayo ni asilimia 12.9 ambapo wengi wao ni wale wenye elimu ya juu,” amesema.
Ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha ujenzi wa vyuo 65 vya ufundi unakamilika haraka.
Waziri Mkuu amesema ukamilishwaji wa vyuo hivyo vinavyojengwa na Serikali unalenga kutimiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha Watanzania kiujuzi.
“Ujenzi wa vyuo hivi ukikamilika, VETA itakuwa na vyuo 145 katika ngazi ya Mikoa yote 26 na Wilaya zote nchini. Vilevile, katika vyuo 80 vilivyopo, vyuo 30 vilikamilishwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita . Tuna kila sababu ya kumpongeza Rais kwa kazi kubwa anayowafanyia Watanzania,” amesema.

Pia Waziri Mkuu ameitaka VETA ihakikishe inatangaza fursa za mafunzo zilizopo ili vijana haswa wa vijijini waweze kuzitumia.
“Inawezekana kabisa kuwa, wapo vijana katika maeneo mbalimbali nchini haswa ya vijijini ambao hawana taarifa ya fursa za mafunzo zilizopo,” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema wanaendelea kutekeleza agizo la Rais Samia la ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya zote.
Pia Mkenda amesema pamoja na ujenzi wa vyuo, wanaimarisha mfumo wa utoaji wa elimu kuendana na mazingira ikiwa ni pamoja na kuimarisha magusiano baina ya VETA, wazalishaji na viwanda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore amesema wataendelea kutoa elimu ya ufundi stadi pamoja na kusimamia bunifu na teknolojia mbalimbali.
Ameishukuru serikali kwa kuweka mkazo ili watanzania wawe na ujuzi utakaowawwzesha kupata kipato