– Zaidi ya Bilioni 1.6 zapatikana
Na Mwandishi Wetu
DODOMA:WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani ijulikanayo kama Mei Mosi, yanahamasisha utoaji wa haki za wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi na ustawi wa wafanyakazi kwa ujumla.
Majaliwa ameyasema hayo jana usiku, Aprili 5, 2025 katika hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuchangisha fedha za kugharamia maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Singida. Hafla hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Royal Village jijini Dodoma.

Amesema dhumuni lingine la maadhimisho hayo ni kutambua na kuenzi michango ya wafanyakazi katika maendeleo ya jamii na uchumi.
Amesema Mei Mosi ni fursa ya kuonesha mshikamano kati ya wafanyakazi na kuhimiza usawa na haki katika maeneo ya kazi duniani kote.

Waziri Mkuu amesema mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hafla hiyo jumla ya Sh. Bilioni 1.62 zilikusanywa zikiwa ni ahadi na fedha taslimu, lengo lilikuwa ni kukusanya sh milioni 832.8.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete, rais wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamuhokya, Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Martha Mlata.