Na Danson Kaijage
DODOMA: SEKTA ya Madini imekusanya Maduhuli ya kiasi cha Sh. Trilioni moja ikiwa imebaki siku moja tu kukamilisha Mwaka wa Fedha 2024/25.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba amesema hayo wakati akifunga Bonanza lililowakutanisha pamoja watumishi wa Wizara na taasisi ambapo wameshiriki katika michezo mbalimbali.
Amesema katika Mwaka wa Fedha 2024/25 Sekta ya Madini ilipangiwa kukusanya shilingi trilioni moja ambazo zimeingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
“Tumeweza kukusanya trilioni moja na ‘point’ bila kuwepo mgodi mpya, hakuna mwaka huko nyuma tuliosogelea Sh. Bilioni 900 lakini mwaka huu tumeweza kukusanya kiasi hicho hii ikiwa ni sawa na wastani wa kukusanya Sh. Bilioni 84 kila mwezi,” amesema.
Amesema mwenendo mzuri wa ukusanyaji wa fedha umeifanya wizara kupangiwa kukusanya Sh. Trilioni 1.2 , hivyo, kuwataka watumishi kuongeza bidii ili Sekta ya madini iwe moja ya taasisi ambazo zitaongeza mapato ya ndani ya nchi yatakayoiwezesha nchi kujitegemea.
Kutokana na mafanikio hayo, Samamba amewapongeza watumishi wote wa Wizara ya Madini na taasisi zake na kueleza kuwa, mafanikio hayo yametokana na mchango wa kila mtumishi kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Amewataka kuendeleza mshikamano na kufanya kazi kwa weledi ili Sekta ya Madini iendelee kutoa manufaa ya kiuchumi kwa Taifa.
Pia amepongeza Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ( BoT) kuanza kununua dhahabu kama akiba ya taifa na kusema suala hilo si dogo.
Amemwagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kuweka utaratibu wa kuwa na mabonanza yasiyopungua mannne Kwa mwaka kuendelea kujenga umoja na mshikamano baina ya watumishi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Tume ya Madini Dkt Janeth Lekashingo amewataka watumishi kuendelea kujenga uhusiano na mawasiliano miongoni mwao huku akisititiza kujenga tabia ya kufanya mazoezi.