Na Lucy Ngowi
MAABARA za Fizikia, Kemia na Biolojia zilizogharimu Sh. Milioni 180 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kakonko, Kigoma zimechochea hamasa kubwa ya kitaaluma kwa wanafunzi.
Maabara hizo zimejengwa kwa ufadhili wa Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) kwa kushirikiana na Mfuko wa Elimu wa Taifa (TEA). Shule hiyo ina wanafunzi 270 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Mkuu wa shule ya Kakonko, Anatoria Nkabo, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza hamasa ya wanafunzi kufanya vizuri zaidi katika masomo ya sayansi kutokana na mazingira bora na rafiki ya kujifunzia kwa vitendo.

“Kwa kupata mradi huu, tunakwenda kuongeza ufaulu. Tunatarajia nusu ya wanafunzi watakaoingia kidato cha nne wapate daraja la kwanza katika mitihani yao ya mwisho,” amesema.
Mwalimu wa Kemia na Biolojia, Nikolous Kayombo, amesema kuwa walifundisha masomo hayo kwa nadharia pekee, lakini sasa, kupitia maabara hizo wanafunzi wataweza kujifunza kwa vitendo, hivyo kuongeza uelewa na ufaulu wao.
Wanafunzi Zulfa Twaha wa Kidato cha Kwanza, Happines Amosi (Kidato cha Tatu), na Sharifat Hamad walitoa shukrani zao kwa UNICEF na TEA kwa kuwapatia maabara hizo muhimu.
Walisema maabara hizo zinawawezesha kufanya majaribio mengi ya masomo ya sayansi, jambo linalochochea mafanikio yao kitaaluma.
Mbali na maabara, TEA pia ilitoa ufadhili wa ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 mwaka 2022/2023, kwa gharama ya zaidi ya Sh. milioni 142.9.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2022 ina jumla ya wanafunzi 274, na mwaka 2025 inatarajia kudahili wanafunzi wengine 100 wa kidato cha kwanza, jambo linaloashiria maendeleo endelevu shuleni hapo.