Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI kwa kushirikiana na Taasisi ya Tokushukai kutoka Japan pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), imepanga kujenga Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Figo na Mafunzo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma.
Akizungumza, katika Ofisi za Wizara ya Afya jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ismail Rumatila, amesema Serikali ipo tayari kupokea na kushirikiana na Taasisi ya Tokushukai katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati.

Rumatila amesema lengo mahsusi la mradi huo ni kuanzisha kituo cha umahiri katika magonjwa ya figo na upandikizaji wa figo kitakachotoa huduma za matibabu, mafunzo na tafiti kwa wataalam wa afya nchini.
Rumatila ameongeza kuwa mradi huo unakadiriwa kugharimu Sh Bilioni 44.9, ambapo Shirika la Tokushukai litachangia Sh Bilioni 28 kwa ajili ya ujenzi na ununuzi wa kifaa cha matibabu ya mishipa ya damu kwenye ubongo, huku Serikali ya Tanzania ikigharamia Sh Bilioni 16.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, mafunzo, na ajira kwa wataalam wa afya.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi kutoka Shirika la Tokushukai, Yukihiro Noguchi, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za figo na kuimarisha miundombinu ya afya nchini.

Kituo hicho kinatarajiwa kuimarisha huduma za upandikizaji figo nchini, kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya, kufanya tafiti, na kupunguza gharama kwa wagonjwa wanaolazimika kusafiri nje ya nchi kufuata huduma hizo.

