Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema lugha ya kichina inakuza diplomasia na kuimarisha uhusiano mzuri katika kuwezesha diplomasia ya kiuchumi.
Kipanga amesema hayo kwenye hafla ya Mashindano ya Kimataifa ya Walimu wa Lugha ya Kichina nchini Tanzania yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Amesema lugha hiyo ilianza kufundishwa nchini tangu mwaka 2013 kupitia Taasisi ya Kichina ya UDSM.
Amesema kujifunza lugha hiyo kutafungua milango ya fursa pamoja na mawasiliano rahisi na Wachina katika nyanja mbalimbali.
“Kwa kujihusisha na mawasiliano kama haya, unafungua milango ya maendeleo yako ya elimu, taaluma ya biashara na kukuza utalii wa lugha. Hivyo kutokana na diplomasia ya lugha unajenga pia diplomasia ya kiuchumi,” amesema.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema kujifunza lugha hiyo na kusoma nchini China kunazidi kuwa maarufu kwa Watanzania.
“Shindano hili linaweza kutoa maarifa zaidi na mambo mapya kuhusu mbinu za kufundishia, kuboresha ustadi wa kufundisha kupitia jukwaa hili na kutangaza kwa ustadi uzuri wa lugha ya Kichina kwa wanafunzi wa Kitanzania,” amesema/
Makamu Mkuu chuoni hapo, Profesa William Anangisye amesema kuwa taasisi ya kichina chuoni hapo ilianzishwa chini ya makubaliano kati ya Chuo Kikuu na makao makuu yaliyoko Hanban na Chuo Kikuu cha Kawaida cha Zhejian nchini China ili kuwezesha lugha ya Kichina.
Profesa Anangisye amesema taasisi hiyo inalenga kukidhi haja ya Tanzania ya kuelewa utamaduni, teknolojia na ujuzi wa lugha ya Kichina na kuongeza maelewano kati ya watu wa China na Tanzania.
Vile vile amesema taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi kama jukwaa la mabadilishano ya kijamii, kisiasa na kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Amesema taasisi hiyo imewaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu na makampuni nchini Tanzania kabla ya kuhitimu elimu yao.
Amesema wafanyakazi wa Taasisi hiyo wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa vijana wa Kitanzania wanajifunza lugha ya Kichina ili kuboresha uwezo wao wa kiushindani katika kukuza taaluma na kujiendeleza pia.
“Juhudi zetu za pamoja zimewawezesha wanafunzi wetu na kitivo, kupanua mtandao wetu wa kimataifa na kuimarisha sifa yetu ndani na nje ya Tanzania,”amesema.
Awali, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Zhang Xiaozhen amesema mashindano hayo yalishirikisha walimu 54 wa China kutoka nchi 11. Kutoka Tanzania, Zambia, Rwanda, Msumbiji, Mali, Madagascar, Liberia, Kenya, Ghana, Misri na Cameroon.
Amewahimiza walimu zaidi wa China kushiriki katika shindano hilo ili kuongeza dhana za kitaaluma, ujuzi wa maarifa na utendaji wa walimu wa ndani wa China barani Afrika.