Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Kibamba kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Edward Kinabo, amewataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua ili aweze kutatua tatizo la muda mrefu la maji.
Akizungumza katika Kata ya Saranga, Kinabo amesema serikali ya CCM imeshindwa kutatua changamoto hiyo na haina mpango wa kufanya hivyo. “Wanakibamba nichagueni muhanga mwenzenu, msimchague mkazi wa Oysterbay, maana hamtatoboa,” amesema.

Kinabo ameeleza kuwa ameamua kugombea kwa sababu anaifahamu vizuri kero ya maji akiwa mkazi wa Goba, anayenunua maji ya madumu kama wakazi wengine wa Kibamba.
Amesisitiza kuwa barabara ya Morogoro inayopitisha makontena ya biashara kubwa haijawanufaisha wakazi wa Kibamba kwani hakuna barabara za lami wala huduma za msingi kama maji.
“Nimegombea Kibamba ili kumaliza shida ya maji. Jimbo hili ndilo la kwanza kutoka mkoa wa Pwani lilipo chanzo cha maji cha Ruvu, lakini maji yanaelekezwa Oysterbay badala ya Kibamba,” amesema.
Amewaomba wananchi kuipiga chini CCM na kuichagua CHAUMMA, akisisitiza kuwa ana uzoefu wa kuandaa miswada na kuuliza maswali bungeni. “Nitumeni nikasukume maji,” ameeleza.

Pia amemwomba mgombea urais wa chama chake kuhakikisha anatenga ruzuku kwa ajili ya miundombinu ya maji, akibainisha kuwa licha ya ushuru wa shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta kutozwa kwa ajili ya miundombinu, bado Kibamba haina barabara zinazopitika.
“Nagombea jimbo hili ili tukarabati barabara za mitaani, hususani Kibamba, kama ilivyo Mwananyamara na Kinondoni ambapo angalau zipo za kupakazia,” amesema.
Kinabo amedai kuwa Halmashauri ya Ubungo inakusanya jumla ya shilingi bilioni 131 kwa mwezi kwa ajili ya maendeleo, lakini wananchi wa Kibamba hawajanufaika nazo. Aliongeza kuwa sera ya ubwabwa siyo masihara, kwani shule bado zinachangia chakula na madawati, licha ya mapato ya madini.
“Nataka serikali ya CHAUMMA iongeze ruzuku kutoka sh. 10,000 hadi 30,000,” amesisitiza.
Akizungumzia mgombea wa CCM, Anjela Kairuki, Kinabo alihoji ufanisi wake, akidai kuwa mtangulizi wake, Issa Mtemvu, alishindwa kuwaletea maendeleo. “Kama Kairuki amekuwa Waziri wa TAMISEMI, jiulizeni ametufanyia nini wakazi wa Kibamba?,” amesema.