Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: UTUMIAJI wa maji kidogo katika ulimaji wa zao la mpunga unapunguza uzalishaji wa gesi kutoka katika zao hilo, pia kuwezesha maji mengine kutumiwa na wengine.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Thomas Bwana amesema hayo katika kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu pamoja na maonesho linalomalizika jijini Dar es Salaam, ambalo liliandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Dkt. Bwana amesema utumiaji huo wa maji kidogo unafanywa kupitia Kilimo Shadidi cha mpunga.
” Kwa kitendo cha kutumia maji kidogo unapunguza uzalishaji gesi kutoka katika mpunga, pili unasaidia haya maji kidogo unayotumia, maji mengine yanaweza yakatumika na watu wengine wanaolima mpunga,” amesema.
Amesema kwa kutumia teknolojia za kisasa katika kilimo, TARI ina sehemu ambayo inachangia kupunguza uzalishaji gesi.
” Kwa mfano tunapokuwa tunakilima kilimo cha mpunga na kujaza maji mengi, tunazalisha gesi aina ya mithel, sasa sisi katika TARI tuna kilimo shadidi ambacho kinatumia maji kidogo,” amesema.
Amezungumzia pia jinsi taasisi hiyo inavyofanya tafiti mbalimbali ili kuwa na teknolojia zinazokabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema TARI ina tafiti aina mbalimbali za mbegu ambazo ni himilivu pia kwa magonjwa na wadudu.