Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, amewaasa wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho ambacho amelitaja kuwa bora kuliko vyuo vyote nchini.
Kikwete aliwaasa hayo baada ya kuhitimishwa kwa Mahafali ya 55, duru ya nne, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

“Tunawapongeza na kuwatakia kila la heri katika shughuli mbalimbali. Pia endeleeni kuwa mabalozi wazuri wa chuo hiki, ambacho ni cha kwanza kuanzishwa na kinaendelea kuwa cha kwanza katika masomo,” amesema Kikwete.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye, amesema chuo kinaendelea na kazi ya mapitio, uhakiki, uidhinishaji na maombi ya ithibati ya mitaala ya programu mbalimbali.
Amesema zaidi ya mitaala 250 imepitiwa na inatarajiwa kuwasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya kupitishwa, ambapo takribani mitaala 242 ya ngazi ya shahada ya awali na uzamili tayari imewasilishwa.
“Hadi sasa, mitaala 49 imepata ithibati kwa mwaka 2025/26. Miongoni mwa programu mpya zilizopata ithibati ni shahada ya awali ya sayansi katika fizikia, na shahada ya umahiri ya fizikia ya tiba.

“Kutunuku shahada na stashahada mwaka 2025, wanataaluma 92 ambao Mlimani 68, MUCE 18, DUCE 6, walipanda madaraja kutoka wahadhiri kuwa wahadhiri waandamizi, kutoka wahadhiri waandamizi kuwa Profesa Washiriki, na kutoka Profesa Washiriki kuwa Profesa,” amesema.
Profesa Anangisye ameongeza kuwa katika duru hiyo ya nne ya Mahafali ya 55, wahitimu 2,046 wamehudhurishwa, wakiwemo: shahada za uzamivu 65, za umahiri 522, za uzamili 26, za awali 1,291, stashahada 126 na astashahada 16.
Ameasa wahitimu kutumia elimu waliyopata kuleta faida kwa Watanzania, akisisitiza kwamba chuo kina jukumu la kuhakikisha masomo yanayofundishwa yanaendana na mahitaji ya soko ili kupunguza changamoto za ajira na kuwapa wanafunzi uwezo wa kujiajiri mara wanapohitimu.

Profesa huyo pia amesema, endapo ajira za serikalini au kutoka sekta binafsi zitachelewa kupatikana, wahitimu wawe wepesi kuangalia sehemu nyingine ambapo maarifa na ujuzi wao unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Balozi Mwanaidi Maajar, amepongeza wahitimu hao akisema ni siku yao ya mwisho ya safari yao kitaaluma, bali ni mwanzo wa safari mpya iliyojaa fursa, majukumu na nafasi ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii na ulimwengu kwa ujumla.





