Na Danson Kaijage
DODOMA: FAMILIA ya aliyekuwa Spika wa Bunge marehemu Job Ndugai, imepinga uvumi unaoenea mitandaoni kuhusu kifo cha ndugu yao.
Mdogo wa marehemu, Machite Mgulambwa, akizungumza na mwandishi wa habari hii amesema kuwa, familia inakanusha vikali madai kuwa kifo hicho kilihusishwa na vikundi au mtu yeyote, akisema ni mapenzi ya Mungu.
Amesema kuwa baadhi ya watu wanadai kifo cha Ndugai si cha kawaida, jambo ambalo familia inaliona kama uchochezi usio na msingi unaolenga kuleta migogoro isiyo ya lazima.
“Ndugai alikuwa akisumbuliwa na mafua sugu kwa muda mrefu, hasa alipopata mavumbi au viyoyozi,” amesema Machite, akibainisha kuwa hali hiyo ilisababisha shida kubwa kiafya kwa marehemu.
Kuhusu mahali pa maziko, Machite amefafanua kuwa awali Ndugai alipendelea kuzikwa kijijini kwa mama yake, Ibwaga, lakini baadaye aliamua kuzikwa katika shamba lake binafsi la Mandumba ili kuondoa mivutano ya kifamilia, kwani hakutaka kuonekana kama anamtenga baba yake.
Amesema kwenye shamba la marehemu alikuwa akilitumia kwa kilimo, ufugaji na pia alijenga kiwanda cha kubangua korosho.
Familia hiyo imewaomba Watanzania kupuuza taarifa zisizo sahihi na kuwaacha waombolezaji waendelee kuomboleza kwa amani.