Na Lucy Ngowi
MBEYA: KATIBU Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Zena Ahmed Said, amezitaka taasisi za dini pamoja na vyuo vikuu, kuhakikisha zinakuwa na wataalamu wa ushauri nasaha kwa ajili ya kuwasaidia vijana wanaokumbwa na msongo wa mawazo.
Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Kitaifa la Vijana lililofanyika mkoani Mbeya, Zena amesisitiza kuwa afya ya akili kwa vijana imeendelea kuwa changamoto kubwa, jambo linalohitaji juhudi za pamoja kutoka kwa jamii, taasisi za elimu, na viongozi wa dini.
“Vijana wanapokumbwa na changamoto za kisaikolojia, ni muhimu wawe na sehemu salama ya kupata ushauri. Vyuo na taasisi za dini zina nafasi kubwa ya kujenga kizazi chenye mtazamo chanya wa maisha,” amesema.
Ameeleza kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, bangi, gundi, na hata dawa za usingizi za hospitali, kutokana na msongo wa mawazo na ukosefu wa mwelekeo.
Katika kongamano hilo, amewaonya vijana dhidi ya kujilinganisha na wengine kupitia mitandao ya kijamii, akisema hali hiyo inachochea hisia za matamanio na kusababisha msongo wa mawazo.
“Mitandao ya kijamii haioneshi uhalisia wa maisha ya watu. Wengine wanaopost nyumba au magari si yao, lakini ukianza kujilinganisha nao, unajikuta unaathirika kisaikolojia,” amesema.
Zena pia amewashauri vijana kuwa makini na kila uamuzi wanaoufanya, kwani kila hatua waliyochukua ina athari nzuri au mbaya kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Aidha, aliwataka vijana kujiepusha na tabia ya kufuatilia taarifa mbaya mtandaoni au kwenye vyombo vya habari, kama vile migogoro na vita vya kimataifa, kwani huongeza mzigo wa kiakili na kuchochea wasiwasi usio wa lazima.
“Kuna watu ambao kila siku wanafuatilia taarifa mbaya vita, majanga, au migogoro hali hii huwajaza hofu na kuwafanya waishi kwa msongo. Jifunze kuchuja taarifa unazozipokea,” amesema.
Kongamano hilo la vijana lilikutanisha washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kujadili changamoto na fursa zinazowakabili vijana katika dunia ya sasa, ikiwemo suala la afya ya akili, mitandao ya kijamii, ajira na maadili.