Na Lucy Lyatuu
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, ameliagiza Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kuhakikisha inaleta mapinduzi makubwa ya viwanda kwa kufungua viwanda vingi na kutengeneza fursa nyingi hususani kwa vijana.
Aidha amelitaka kuongeza kasi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya viwanda.
Katambi ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kikazi katika makao ya shirika hilo, ambapo alisisitiza umuhimu wa NDC kusimamia kwa umakini maeneo yote yaliyo chini ya dhamana yake lakini kufanya kazi kwa kasi kubwa na yenye weledi.
Amesema Serikali imejipanga kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika viwanda, ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa mitaji na ushauri wa kibiashara, kwa lengo la kupanua wigo wa ajira hasa kwa vijana.

Amefafanua kuwa mpango wa Serikali ni kuleta mageuzi makubwa ya viwanda kuanzia vidogo, vya kati hadi vikubwa, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
“NDC ilenge kuwa na viwanda vidogo sana, vidogo vya kati, n ahata vikubwa huku ikihakikisha kuwa viwanda vilivyodorora vinafufuliwa kwa haraka ikiwa ni tija ya kuongeza viwanda zaidi,” amesema.
Aidha, amehimiza mshikamano, mashauriano ya mara kwa mara na kuondoa urasimu usio wa lazima ndani ya shirika, akisisitiza kuwa NDC inapaswa kuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi badala ya kuwa kikwazo.
Ameongeza kuwa mafanikio ya kiuchumi ya nchi yoyote yanategemea uwepo wa viwanda imara vinavyoweza kuzalisha ajira na kuongeza thamani ya rasilimali zake.
Awali akizungumza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Valentine Simkoko, amesema shirika hilo linasimamia miradi mbalimbali ya kimkakati na linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi.
Aliitaja baadhi ya miradi inayosimamiwa na NDC kuwa ni Pamoja na Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda ya Engareka, pamoja na tathmini ya mali za wananchi wanaohusika katika miradi ya makaa ya mawe Katewaka na chuma ghafi cha Maganga Matitu.
Simkoko ameongeza NDC pia imeingia mikataba ya ubia na wawekezaji katika mradi wa chuma wa Maganga Matitu, pamoja na kusaini mkataba na kampuni ya Labiofam S.A. kwa ajili ya kuhamisha teknolojia ya uzalishaji wa mbolea hai nchini.

