Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, ameutaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuboresha utoaji wa huduma kwa kuhakikisha hauwi kikwazo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, bali unachochea urasimishaji wa biashara na ukuaji wa uchumi.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika ofisi za BRELA, Katambi amesema wawekezaji wanaokidhi masharti ya kisheria wanapaswa kupewa mwongozo wa haraka na sahihi, badala ya kukumbana na urasimu unaokwamisha juhudi zao.
Amesisitiza pia umuhimu wa wakala huo kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zake ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
Katambi ameeleza kuwa serikali inaweka mkazo mkubwa kwa ajira za vijana, hivyo sekta ya viwanda na biashara zinapaswa kuwa mhimili muhimu wa kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira na kuongeza mchango wake katika pato la taifa.
Aidha, ameitaka BRELA kufanya tathmini ya kampuni zote zilizosajiliwa ili kubaini zinazofanya kazi na zisizofanya kazi, pamoja na kuboresha mifumo ya huduma kwa wateja kwa kuwashirikisha wahudumu na kutumia lugha yenye staha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki na Ubunifu wa BRELA, Loy Mhando, amesema wakala huo utazingatia maelekezo yote yaliyotolewa kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

