Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Viti Maalum, Dkt. Neema Majule, amehoji Serikali kuhusu mpango wa kusajili wawekezaji wote nchini kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA), hatua inayolenga kuwa na kanzidata sahihi ya uwekezaji.
Akizungumza bungeni, Dkt. Majule ameitaka Serikali kufafanua mikakati yake kuhakikisha wawekezaji wote, wa ndani na wa nje, wanajiandikisha rasmi.
Lengo ni kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga na kusimamia uchumi wa Taifa.
Akijibu, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, amesema TISEZA inaendelea kusajili miradi ya uwekezaji kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, ikiwemo kiwango cha mtaji.
Amesema hadi sasa, Serikali kupitia TISEZA imesajili miradi 14,209 na kutoa vyeti vya utambuzi.
“Mheshimiwa Spika, katika kuendana na maendeleo ya teknolojia ya kidigitali, TISEZA imekamilisha ujenzi wa Mfumo wa Kanzidata ya Taifa ya Uwekezaji wa Sekta Binafsi, utakaounganisha mifumo ya taasisi mbalimbali zinazohusika na usajili wa makampuni ya wawekezaji,” amesema Dkt. Chaya.
Ameongeza kuwa mfumo huo utaboresha upatikanaji wa takwimu sahihi, hususan kuhusu mitaji iliyowekezwa na ajira zinazozalishwa na sekta binafsi.
Serikali pia inaendelea na kampeni ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani kupitia wazawa, sambamba na kuwahamasisha wawekezaji wasiosajiliwa kujiandikisha rasmi.
Kuhusu vigezo vya usajili, Dkt. Chaya amesema wawekezaji wazawa wanapaswa kuwa na mtaji wa angalau dola 50,000 (takriban Sh. milioni 125), huku wawekezaji wa kimkakati wa ndani wakitakiwa kuwa na dola milioni 50.
Kwa wawekezaji wa nje, mtaji wa chini ni dola 500,000 kwa wale wa kawaida na dola milioni 500 kwa wawekezaji wa kimkakati.
Aidha, Naibu Waziri amebainisha kuwa Serikali imeweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kuwavutia wawekezaji zaidi kuwekeza na kujisajili rasmi kupitia TISEZA.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwazi, ufuatiliaji na mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa.

