Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KANISA la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, limetumia Sh. Milioni 470.8 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika Shule ya Msingi Kibamba iliyopo Halmashauri ya Ubungo Dar es Salaam.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Genuine Kahatano amesema hayo katika taarifa yake ya shukrani aliyoisoma kwa uongozi wa Kanisa hilo, viongozi wa serikali, walimu pamoja na wanafunzi, muda mfupi kabla ya kukabidhiwa miundombinu hiyo.
Kahatano ametaja miundombinu hiyo iliyojengwa na kukarabatiwa kuwa ni
vyumba vya madarasa tisa vikiwa na umeme, ofisi mbili ndogo za walimu na Ofisi moja kubwa ya walimu.

Pia vyoo vya wanafunzi na mnara wa matenki ya maji kwa thamani ya sh milioni 329.5.
“Shule ya msingi Kibamba, tunatoa chozi la furaha tukisema asanteni sana kwa kazi kubwa isiyo na mfano mliyoifanya. Mwenyezi Mungu azidi kuwabariki kwa kazi nzuri,”amesema.
Naye Rais wa Kanisa hilo, Juventinus Rubona amesema miradi iliyokamilika imegharimu Sh. Milioni 753.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni wa shule hiyo ya Kibamba, Kituo cha Afya Kimara na Kituo cha Afya Makuburi.
Amesema miradi ya sasa inayotarajiwa kukamilika ina thamani ya Sh. Milioni 522.
Katibu Tawala wa Wilaya hiyo ya Ubungo, Hassan Mkwawa amelishukuru Kanisa hilo kwa msaada walioutoa katika shule hiyo na maeneo mengine.

Ameagiza miundombinu hiyo itunzwe ili kizazi kijacho kiweze kuitumia.