Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Palamagamba Kabudi, amesema kutosoma vitabu kunaweza kufanya ubongo kusinyaa na kupunguza uwezo wa kufikiri.
Kabudi amesema maelezo hayo ni kwa mujibu wa wataalam wa afya ya akili.
Amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania yanayoendelea Dar es Salaam.

“Vitabu ni tiba, husadia kuongeza maarifa, kuboresha fikra, kuimarisha msamiati na ufasaha wa lugha, kuongeza ubunifu, kupunguza msongo wa mawazo na kukuza nidhamu,” amesema.
Ametoa wito wa kujengea watoto utamaduni wa kusoma vitabu na kuhimiza ubunifu katika uchapishaji.
Kabudi amesema maktaba ni taasisi muhimu kwa taifa lolote linalojitambua, hivyo kuna haja ya kuimarisha uhusiano kati ya maktaba na waandishi wa vitabu ili kuendeleza maktaba za taifa.
Pia amewataka wadau wa lugha ya Kiswahili kutumia majukwaa yaliyopo kuboresha mchango wao katika kutunza uchumi na tamaduni.
Amesema sekta ya vitabu ni chanzo cha ajira na kipato kupitia uandishi, uchapishaji na uuzaji wa vitabu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba, Dkt. Mboni Ruzegea, amesema maadhimisho hayo yamelenga kukumbushana umuhimu wa vitabu nchini.
Amesema vitabu vinachangia kujenga ujirani mwema, diplomasia na uchumi.
Pia ameitaka serikali kuendelea kuipa nguvu sekta ya vitabu kwa kuwa bila vitabu na maktaba imara, haiwezekani kujenga uchumi na maarifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji wa Vitabu (PATA), Hermes Damian, amemwomba Waziri Kabudi kuwasaidia katika kuimarisha sekta ya vitabu na kuwezesha utungaji wa sera madhubuti ya uandishi na usomaji wa vitabu.
Amesema sera hiyo itasaidia kujenga taifa linalovithamini vitabu na kutoa mchango wa kifikra, maarifa na weledi katika nyanja mbalimbali za maisha na maendeleo.
Pia ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza utegemezi wa taarifa zilizotafuniwa tayari.



