Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHAMA cha Wafanyakazi Katika Vyombo vya Habari nchini(JOWUTA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi Duniani(IFJ) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu(THRDC) wanatarajia kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini jinsi ya kuripoti uchaguzi mkuu wakiwa salama.
Mafunzo hayo ambayo yanaratibiwa na JOWUTA katika awamu ya kwanza yanatarajiwa kufanyika Aprili 2025 katika Kanda tatu nchini, ambazo ni Pwani , Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini ambayo itaandamana na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uhuru wa habari ambayo itafanyika jijini Arusha.

Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma amesema hayo katika taarifa aliyoitoa baada ya viongozi wa JOWUTA kutembelea Makao Makuu ya THRDC jijini Dar es salaam, kufanya mazungumzo na Mratibu wa kutaifa wa mtandao huo, Onesmo Ole Ngurumwa.
Juma amesema katika mkutano wa waandishi wa habari Afrika uliofanyika nchini Senegal na baadae Rwanda, JOWUTA imeomba IFJ na Shirikisho la Waandishi Afrika(FAJ) kusaidia mafunzo kwa wanahabari Tanzania ili waweze kuripoti uchaguzi kwa haki na salama.
“Niliomba watusaidie mafunzo na baada ya majadiliano baina yao IFJ ikakubali kugharamia sehemu ya mafunzo,” amesema.
Amesema kutokana na mafunzo kuhitaji gharama kubwa JOWUTA iliamua kuanza kutafuta wadau wengine kushirikiana nao wakiwepo THRDC.
Naye Mratibu wa THRDC Ngurumwa amesema THRDC itachangia sehemu ya gharama za kufanikisha mafunzo kwa wanahabari nchini.
“Sisi kama wadau wakubwa wa watetezi wa haki za binadamu wakiwepo waandishi wa habari tutachangia mafunzo haya ili waandishi waweze kuripoti vyema uchaguzi mkuu kwa haki,bila upendeleo lakini wakibaki salama,” amesema.
Amesema THRDC kwa muda sasa imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa waandishi ikiwepo sheria za uchaguzi lakini pia mafunzo ya ulinzi na usalama kazini.
Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA, Seleman Msuya amesema JOWUTA ndio chama pekee kinachotambulika kisheria nchini ambacho kinatetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari na masuala ya mazingira bora ya kazi zao.
Amesema THRDC kukubali kufanya kazi na JOWUTA hawajakosea na watakuwa pia wametimiza wajibu wao kuwasaidia watetezi wa haki za binadamu kufanyakazi katika mazingira salama.
Hata hivyo alitoa wito kwa wadau wengine kusaidia wanahabari kupitia JOWUTA ambayo ina zaidi ya wanachama 400 nchi nzima.