Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE mteule wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, Jackline Chrisant Mzindakaya, amesema uteuzi wa Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania ni chaguo sahihi.
Amesema hayo muda mfupi baada ya kuthibitishwa jina hilo na wabunge jijini Dodoma.
Amesema Mwigulu ni kiongozi mchapakazi, mwenye maono na ambaye amekuwa sehemu muhimu katika kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Vilevile, amehusishwa katika uandaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, ikiwemo kujadili vipaumbele vya maendeleo vya kiuchumi, kijamii na kisiasa vinavyoendana na matarajio ya Watanzania.
Mzindakaya pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupendekeza jina la Mwigulu Nchemba kushika nafasi hiyo, pamoja na wabunge wote waliopitisha azimio hilo kwa kura za kishindo.
Amesema anamfahamu Mwigulu kama kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika nafasi mbalimbali za chama na serikali, na kwamba amekuwa akifanya kazi kwa uadilifu na ufanisi.
Anaamini ushiriki wake katika kuandaa ilani mpya na dira ya maendeleo utasaidia kuvusha taifa kimaendeleo.
Aidha, Mzindakaya ameeleza kufurahishwa na hotuba ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba, hasa sehemu iliyogusia masuala ya vijana. Amesema kauli ya Waziri Mkuu kwamba atatoa kipaumbele katika ajira kwa vijana imegusa mioyo ya wengi, akiwemo yeye kama kijana anayewakilisha vijana wa Tanzania.
Ameongeza ana imani kuwa Waziri Mkuu Nchemba ataboresha maisha ya Watanzania wa kipato cha chini, kwani anafahamu changamoto wanazokabiliana nazo.

