Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM:“MADHUMUNI yetu ni kuendelea kuwa taasisi kwenye eneo la kilimo na tafiti Afrika. Kwamba watu wakituangalia waweze kuja kufanya tafiti na sisi na kuleta mabadiliko katika bara letu la Afrika,”.
Ofisa Mawasiliano wa Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA), Gloriana Ndibalema amesema hayo alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania kuhusu taasisi hiyo.
Amesema taasisi hiyo imekuwa na mkakati wa mwaka 2030 wa kuendeleza chakula, kuongeza nafasi kwa wanawake na vijana, ili kusaidia kupata kazi zinazotokana na kilimo.
Pia amesema taasisi hiyo inapima afya ya udongo kama hauna afya ama virutubisho, kwa kuwa bila kufanya hivya kilimo hakiwezi kuwa sawa.
“Kama umeboresha zao lakini udongo hauna afya hautafanikiwa,” amesema Gloriana na kuongeza kuwa nchini Tanzania taasisi hiyo inafanya utafiti katika zao la mihogo na ndizi kwa kuwa na programu inayoboresha ndizi za kupika.
“Watu hawajui ndizi inaweza kuboreshwa. Sasa zinaboreshwa. Kwa Tanzania zinaboreshwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI). Tumeweza kuja na mbegu aina ya TARI Banana. Kuna TARIBAN 1, TARIBAN 2, TARBAN 3 na TARIBAN 4,” amesema.
Amesema katika tafiti wanazofanya wanaangalia wakulima wanataka nini hivyo shughuli zote za kisayansi zinafanyika IITA.
“Tunafanya utafiti unaoweza kukabiliana na magonjwa, pia mbegu inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,” amesema.
Amesema kwenye zao la mihogo wanatafiti mbegu zinazokinzana na magonjwa, na wameshagundua zaidi ya mbegu 20 zinazotumika hapa nchini.