Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) imetajwa kuwa jukwaa muafaka la kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazozikabili nchi wanachama, hususan matatizo ya ukosefu wa amani, usalama na maendeleo endelevu.
Kauli hiyo imetolewa mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Novemba 13 , 2025 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kawaida wa Mawaziri wa ICGLR uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa DRC, Judith Tuluka Suminwa.

Katika mkutano huo, nchi wanachama zimetakiwa kuenzi na kutekeleza kwa dhati Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, ambao unalenga kupatikana kwa amani, usalama na maendeleo ya kweli kupitia umoja, ushirikiano na mshikamano, sambamba na kujitoa kwa hali na mali katika kufikia malengo hayo.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa. Tanzania imeunga mkono ajenda zinazojadiliwa, hususan zile zinazohusu amani na usalama, na imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuchangia juhudi za kurejesha na kudumisha amani katika Kanda.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Waziri Mkuu wa DRC amebainisha kuwa nchi za ICGLR bado hazijafikia malengo ya msingi ya Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya hiyo—ambayo ni amani, usalama na maendeleo.
Ametoa wito kwa nchi wanachama kuongeza umoja, mshikamano na ushirikiano ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto za kiusalama. Aidha, alitaja ukosefu wa rasilimali fedha na miundombinu duni ndani na baina ya nchi wanachama kama sababu zinazochangia kutofikiwa kwa malengo hayo.
Katika hitimisho la hotuba zao, viongozi walisisitiza umuhimu wa nchi za ICGLR kubuni mikakati ya ndani ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili Kanda bila kutegemea msaada wa nje. Pia walihimiza kuimarishwa kwa taasisi za kikanda kwa kuzitengea rasilimali fedha na wataalamu ili ziweze kushughulikia kikamilifu changamoto za amani na usalama.




