Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: SERIKALI imeanza kuwalipa wafanyakazi 465 kati ya 645 wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania ( TALGWU), kupitia mfuko mkuu wa serikali – Hazina.
Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashid Mtima amesema hayo alipozungumza na waandishi wa Habari mkoani Dar es Salaam, na kuongeza kuwa wafanyakazi hao wameanza kulipwa Julai mwaka huu.
Mtima amesema kundi hilo la wafanyakazi awali lililipwa mishahara yao kupitia mapato ya halmashauri.
Amesema TALGWU katika vikao na majadiliano mbalimbali na serikali mara kadhaa ilikuwa ikizungumzia changamoto, kero na kadhia wanazopitia watumishi hao ambao ni wanachama wao.
Amesema watumishi hao wakati wakilipwa na halmashauri, walipitia changamoto za kutolipwa mishahara kwa wakati, kukosa huduma ya matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kutokana na makato kutowasilishwa kwa wakati.
Vile vile kutokukopesheka katika baadhi ya taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na kupata usumbufu mkubwa pindi wanapostaafu kutokana na makato ya michango yao kutokuwasilishwa kwa wakati katika mfuko wa hifadhi ya jamii.
“Hii ni hatua kubwa sana iliyochukuliwa na serikali kwani itaondoa kero za muda mrefu, itaongeza ari na morali ya kufanya kazi.
“Pamoja na pongezi hii tunaiomba tena serikali kuangalia upya na kufanya mchakato ili wanachama wetu 180 waliosalia katika majiji na manispaa ambao bado wanalipwa kwa mapato ya ndani ya halmashauri nao waanze kulipwa kupitia hazina ” amesema.