– Yafungua Kliniki Ya Biashara Kwa Faragha
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Udhibiti wa Ushindani wa Kibiashara (FCC) imetumia jukwaa la maonesho ya biashara kufikisha elimu kwa wadau wa biashara huku ikizindua ‘clinic’ maalumu ya biashara inayotoa ushauri wa faragha kuhusu masuala ya ushindani wa kibiashara na ulinzi wa walaji.
Akizungumza katika maonesho hayo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Hadija Ngasongwa amesema maonesho haya ni fursa muhimu kwa mamlaka hiyo kufikia zaidi ya washiriki 3,500 wa sekta mbalimbali za biashara kwa lengo la kuhamasisha ushindani wenye tija na mazingira bora ya uwekezaji nchini.

“FCC imefungua clinic ya biashara ili kuwawezesha wafanyabiashara hasa wale wadogo na wa】⁰⁰⁰0 kati kupata taarifa sahihi kuhusu sheria za ushindani na haki za walaji kwa faragha kabisa,” amesema.
Amesema FCC imekuwa ikifanya kazi ya kuelimisha umma, kufuatilia mienendo ya soko, pamoja na kudhibiti bidhaa bandia zinazohatarisha afya za walaji na kuathiri ushindani halali wa kibiashara.
Kwa mujibu wa Ngasongwa, Serikali kupitia FCC imeweka mazingira rafiki ya kufanya biashara, jambo linaloendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Amesema Tanzania bado ni mahali salama na bora pa kuwekeza kutokana na mfumo thabiti wa kisheria unaolinda haki za wafanyabiashara wote.
“Sheria zetu ni rafiki kwa wawekezaji, na tunajivunia kuona kwamba sasa Serikali imeweka mazingira mazuri zaidi kwa biashara kushamiri,” amesema.
Amesema FCC inaendelea kufanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kuweka uwiano katika soko na kusaidia biashara ndogo kukua na kufikia ngazi za juu.
Amesema dhamira ya FCC ni kuhakikisha siyo tu wawekezaji kutoka nje wanafaidika na mazingira ya biashara, bali pia wajasiriamali wa ndani wanapata nafasi ya kukuza mitaji yao kupitia ushindani wa haki.
“Tunaamini kuwa kupitia elimu na usimamizi madhubuti wa ushindani, tunaweza kuwawezesha wafanyabiashara wa kati kukua na kuwa wawekezaji wakubwa wa baadaye,” amesema.
Maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la wadau mbalimbali kubadilishana uzoefu na kupata mrejesho kuhusu mazingira ya kibiashara nchini, huku FCC ikichukua hatua ya kuwa karibu zaidi na jamii ya wafanyabiashara kwa vitendo.