Na Lucy Ngowi
DODOMA: MKUU wa Wilaya ya Kongwa ametoa wito kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) kufuatilia na kuzingatia sheria ndogondogo zinazopitishwa katika halmashauri na vijiji, akisema zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika mabadiliko ya sheria kuu za kitaifa.
Amesema hayo alipotembelea banda la LRCT, katika Maonesho ya Nanenane ya Kitaifa yanayoendelea mkoani Dodoma,
Amesema sheria hizo, ingawa zinaweza kuonekana ndogo au za kawaida, ndizo zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja na mara nyingine zinatatua kero kubwa ambazo hazijawekewa sheria katika ngazi ya kitaifa.
“Inawezekana jambo linaonekana ni la kawaida lakini kule chini kwenye jamii linakuwa ndiyo kero kubwa ya wananchi. Halmashauri nyingine hujiwekea sheria ndogondogo ambazo zinafanya vizuri, lakini halmashauri nyingine hazijui kama kuna mahali panafanyika hivyo,” amesema.
Amesisitiza kuwa sheria hizo ndogondogo zinaweza kuchangia katika uundaji wa sheria mama kwa sababu zinatokana na hali halisi ya jamii. Na kutoa mfano wa sheria za mazingira zinazotungwa katika vijiji vya Wilaya ya Kongwa ambazo, kwa mujibu wake, zinaweza kuwa mfano bora kwa halmashauri nyingine nchini.

Naye Wakili kutoka katika tume hiyo, Vick Mbunde amesema kuwa tume hiyo ilianzishwa mwaka 1981 na kuanza kazi rasmi mwaka 1983, ikiwa na jukumu la kufanya mapitio na marekebisho ya sheria mbalimbali nchini.
Amesema licha ya changamoto ya bajeti, tume imefanikiwa kufanya mapitio ya sheria nyingi, zikiwemo:
Sheria ya uchaguzi, Sheria ya mtoto, kufuatia kuongezeka kwa ukatili dhidi ya watoto, Sheria ya vinasaba (DNA), baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa maoni na Sheria zinazohusu sekta ya kilimo,
Mbunde alibainisha kuwa mchakato wa marekebisho ya sheria hufanywa kwa kuangalia mfumo mzima unaohusiana na eneo husika. Kwa mfano, katika sekta ya kilimo, tume huchambua sheria zote zinazogusa sekta hiyo kwa pamoja.
Hata hivyo, amekiri kuwa tume hukumbwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti, hali nayosababisha kufanya mapitio ya sheria chache tu kwa mwaka.
“Kwa mwaka tunaweza kufanya mapitio ya sheria 10 hadi 12, lakini tunazo zaidi ya 400. Kwa mujibu wa utaratibu, sheria inapaswa kufanyiwa tathmini kila baada ya miaka mitano. Kwa hiyo tuko taratibu sana kwa sababu ya bajeti,” amesema,
Pia amesema changamoto nyingine ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika kutoa maoni wakati wa mapitio ya sheria. Alisema wengi hujitokeza kutoa maoni tu endapo suala linawagusa moja kwa moja.
Tume hiyo inaendelea kutumia mbinu mbalimbali kuongeza ushiriki wa wananchi, ikiwemo kupeleka timu katika maeneo ya jamii ili kupata maoni ya moja kwa moja.