Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: Mkoa wa Dar es salaam katika Utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 umeidhinishiwa Sh. Bilioni 68 kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya Barabara ya zaidi ya kilomita 1000.
Aidha lami kilomita 26.04, pamoja na madaraja na Kalavati 38.
Akimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), Ismail Mafita amesema hayo katika Semina ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), iliyofanyika mkoani Dar es Salaam.
Amesema, “Maendeleo ya utekelezaji kwa Mipango ya mwaka 2024/2025 yanahusisha utekelezaji wa kimaumbile na kifedha ambapo utekelezaji hadi kufikia Disemba 2024 wa kimaumbile ni asilimia 53,”.
Pia amesema mkoa wa Dar es Salaam, unatekeleza miradi ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara inayogharamiwa na fedha za mapato ya ndani ya Wakurugenzi ambapo utekelezaji wake umefikia katika hatua mbalimbali.
Amesema barabara nchini ni nguzo muhimu katika sekta ya usafiri na usafirishaji ambayo kwa kiwango kikubwa hutumiwa na watu wote kuanzia wenye vipato vya chini, kati na juu.
Amesema rasilimali barabara ndiyo njia kuu ya usafiri na usafirishaji, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wasafiri na zaidi ya asilimia 80 ya mizigo hutumia njia hiyo.
Amesema barabara ni nyenzo muhimu inayochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku ufanisi wa mipango ya serikali inayolenga maendeleo ya vijijini,
Uzalishaji wa ajira pamoja na maendeleo ya viwanda kwa kiasi kikubwa unachangiwa na ubora wa huduma za usafiri kwa njia ya barabara.
Amesema ndio njia pekee na rahisi inayowaunganisha wazalishaji wa masoko, wafanyakazi na ajira, wanafunzi na shule pamoja na wagonjwa na hospitali.
“Barabara zinatoa mchango muhimu katika kutimiza malengo ya serikali ya kuhakikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.