Na Lucy Ngowi
ARUSHA: MRADI wenye thamani ya Sh. Milioni 156 wa kuzalisha Gesi Asilia kwa kutumia Samadi kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na watumishi, umezinduliwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa adhma ya Serikali kuhakikisha matumizi ya nishati safi na endelevu.

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) kupitia chuo chake cha Arusha, imezindua mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha gesi asilia kiasi cha 50 cc kwa siku.
Pia mradi huo una uwezo wa kutumika kupika chakula cha wanafunzi zaidi ya 400 kwa siku na kutumika katika nyumba sita za walimu pamoja na kantini ya chuo.
Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ledislaus Mnyone ambaye amemwakilisha, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo amesema mradi huo ni juhudi za Serikali kufanikisha mpango wa kuhakikisha matumizi ya nishati safi na endelevu.
“Serikali imejidhatiti kuimarisha matumizi ya nishati safi inayochangia kupunguza utegemezi wa nishati kutoka vyanzo visivyo endelevu kama vile kuni, mkaa na mafuta” amesema Profesa Mnyone.
Amesema mradi huo utaleta manufaa makubwa kwa jamii hasa katika kupunguza uchafuzi wa mazingira na kusaidia katika kutunza rasilimali za asili.

“Nawapongeza sana VETA kwa ubunifu huu, kinachoonekana hapa ni matokeo ya agizo alilolitoa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambalo nyie mmelitekeleza kwa vitendo,
“Naomba mradi huu uwe endelevu na kuondokana na ile kasumba mradi ukishazinduliwa haufuatiliwi hadi unakufa. Hii imekuwa ikiipatia Serikali hasara kubwa sana, na sasa tutakuwa tunafuatilia maendeleo ya miradi hii,”amesema.
Ametoa wito kwa taasisi zilizokuwa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha teknolojia hiyo inasambazwa kote nchini ili kuokoa gharama kubwa ya matumizi ya kuni, lakini pia kuokoa uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini, Anthony Kasore amesema VETA imeanza kutekeleza Mpango wa Serikali katika kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika vyuo vyake hasa katika matumizi ya gesi.
“Kupitia mradi huu tunaenda kupunguza gharama za uendeshaji hasa katika kununua kuni, na mkaa, lakini pia tutahakikisha mradi huu unakuwa endelevu na wenye kuleta matokeo,” Amesema CPA. Kasore.
Hata hivyo Kasore amesema kwa kupita mradi huo ameona kuna umuhimu wa kuanzisha kozi ya ufugaji, hasa ufugaji wa ng’ombe na ili kupata samadi kwa ajili ya kulisha mtambo huo wa gesi asilia.
Ameishukuru Serikali ya Korea Kusini kupitia Wanasayansi na Wahandisi wasio na Mipaka (SEWB) pamoja na Wizara ya Elimu kuwezesha ujenzi wa mradi huo.
Mkurugenzi wa SEWB, Wiin Soo amesema mradi huo ni matokeo ya mazungumzo kati ya ofisi yake na taasisi ya Tume ya Sayansi Teknolojia (COSTECH), ambayo iliomba msaada wa kusaidiwa kujengewa mtambo huo wa mfano ikiwa ni agizo la Rais Samia.