Na Lucy Lyatuu
BENKI Kuu Ya Tanzania (BOT)
imesema watu wengi wanaendelea kuumia kwa kukosa uelewa wa kujua kinachotakiwa, haki zao muhimu na wajibu wao wakati wanapotaka mkopo.
Ofisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka BOT, Deogracious Manyama amesema hayo Dar es Salaam wakati benki hiyo ikiendelea na kampeni ya kuelimisha watanzania kuhusu hatua zinazotakiwa wakati wa kukopa fedha.
Amesema BOT inafanya kampeni kwa sababu licha ya kuwepo kanuni bora, sheria na sera za fedha bado wanaendela kuumia.
” Tumefanya utafiti na kubaini kuwa kinachosababisha kuendelea kuumia ni kwa kukosa uelewa wa kujua vitu gani vya muhimu, haki wakati wanapokwenda kuchukua mkopo” amesema na kuongeza kuwa maumivu hayo hukutana nao wanapokutana na watoa huduma ambao sio waaminifu.
Amesema umekuwepo ushahidi kwamba watanzania wamekuwa wakinyanyasika, kudhulumiwa na kupata hasara nyingi kwenye eneo la mikopo.
” Hivyo BOT imeona hiyo changamoto itatuliwe kwa kutoa elimu kwa umma ambapo wanapita mtaa kwa mtaa kwa mkoa wa Dar es Salaam ili kutoa elimu, ” Amesema na kuongeza kuwa mpaka sasa wameshapitia eneo la Kigamboni, Temeke na Ilala.
Amesema kwa sasa wanaelekea eneo la Kinondoni na Ubungo na kampeni hiyo inapita mtaa kwa mtaa, kitongoji kwa kitongoji lengo likiwa kuelimisha watanzania ili wanapokwenda kukopa wawe na vitu muhimu vya kuzingatia.
Amesema kampeni imekuja ili kuwafikia wananchi wakiwa kwenye maeneo yao ya kazi na kwa siku wanauwezo wa kufikia watu 3000 kwa kuwatumia mabalozi mbalimbali.
Amesema BOT imefanya utafiti nini kinachosababisha kukopa bila kuzingatia mambo muhimu ikiwa ni pamoja na kukopa kwenye taasisi zilizopewa leseni na BOT kwani inakuwa ni rahisi kufuatiliwa pindi inapotoka kwenye mstari na kuweza kurudishwa.
Amesema pia watanzania watambue wanapotaka mkopo kuzingatia vigezo na masharti kwa kusoma mikataba ya mkopo husika, kuielewa na kutafakari vizuri na pia kuchukua nakala ya mkataba anaouingia.
Kadhalika amesema ni muhimu wakati wa kukopa kurejesha kwa wakati na wanapokutana na malalamiko yoyote watoe taarifa kwenye dawati la kupokea malalamiko lililoko BOT.
Amesema pia wanapokopa wakope kwa maendeleo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji ambazo zitasaidia kufanya marejesho.
“Tumekutana na changamoto ya watanzania kukopa na kupeleka fwdha kwenye sherehe hivyo kupitia kampeni hiyo tunaenda kumzindua mtanzania ili ajue vigezo na masharti lengo likiwa kumlinda mlaji” amesema.
Amesema kwa siku 12 zilizobakia kwa mwezi huu kampeni inaelekea Kinondoni na Ubungo na siku za mbeleni wanaweza kufikiria kuifikisha maeneo mengine.