Na Danson Kaijage
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini kupitia CCM, Paschal Chinyeli, ameahidi kutoa chakula bure kwa wazee wote endapo atachaguliwa kuwa mbunge.
Akihutubia mkutano wa CCM Kata ya Nala, Chinyeli amesema anatambua changamoto ya uhaba wa chakula, hivyo atahakikisha visima vinachimbwa ili kuwezesha kilimo cha uhakika na hatimaye wazee kupata chakula bila malipo.
“Nikipata nafasi ya kuwa mbunge, nitahakikisha tunapata visima vya kutosha ili kulima chakula cha kuwatosheleza wazee,” ameahidi Chinyeli.
Amesema pia atatumia uhusiano wake na viongozi wa taasisi mbalimbali nchini, hasa TANESCO, kuhakikisha maeneo yenye changamoto ya umeme yanaunganishwa haraka.
“Nimesoma na Mkurugenzi wa TANESCO. Nikizungumza naye, anatuletea umeme kwa haraka,” amesema.
Katika mkutano huo, mgombea mwingine, Abdulhabib Mwanyemba, amesema atapambana kila sehemu kutafuta maendeleo ya jimbo hilo endapo atapewa ridhaa.
Maswali ya wajumbe wengi yalihusu ajira kwa vijana, miundombinu na upatikanaji wa maji katika kata hiyo.