Na Lucy Ngowi
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari ya Baobab iliyoko Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wamenufaika na elimu ya vitendo ya ujenzi iliyotolewa na Kampuni ya China Communication Construction (CCCC).
Ofisa Elimu Taaluma kutoka Halmashauri ya Bagamoyo, Juma Yusuph ameeleza hayo baada ya kampuni hiyo kuhamasisha wanafunzi hao kuingia kwenye taaluma ya uhandisi wa ujenzi.

“Kwetu sisi ni faraja. Inaleta chachu kwa wanafunzi hususan wanaosoma masomo ya sayansi kwa kuzingatia maendeleo mengi yanakuja kutokana na ufanisi mkubwa katika sayansi.
“Hii itatusaidia kuhamasisha wanafunzi kuwa chachu ya kuweza kufaya vizuri kwenye sayansi, kujiingiza moja kwa moja katika tasnia ya uhandisi kwenye ujenzi wa barabara na mawasiliano,” amesema.
Amesema dunia sasa ipo katika mfumo wa sayansi na teknolojia unaohitaji wanasayansi wengi waweze kufanikisha maendeleo kwani nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na wataalam wa sayansi wanaoweza kufanya miradi mingi itakayoifanya nchi ipige hatua.
Naye Naibu Meneja wa CCCC, Li Yuijang amesema kampuni hiyo imekwenda shuleni hapo kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo utaalam wa ujenzi, na mbinu zitakazowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Mwalimu Mkuu katika shule hiyo ya Baobab, Venance Wangoha amesema wameweza kushuhudia kampuni hiyo ikionyesha kazi inazozifanya nchini kuhusiana na uimarishaji wa miundombinu ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wanafunzi kusoma sayansi.
Amesema wahandisi hao kutoka China wameonyesha vifaa wanavyotumia katika kutengeneza miundombinu kwa wanafunzi.

Mwanafunzi Amor Bayumi amekiri kujifunza njia mbalimbali za kutengeneza madaraja ambayo yatapita juu ya bahari ama katika ardhi ambayo imepata dhoruba ya kimazingira ikiwemo mpasuko wa ardhi.
Pia mwanafunzi mwingine wa kidato cha sita shuleni hapo, Amrat Haishaul amesema kupitia mafunzo hayo, yamewahamasisha kuwa hata kama wanasoma kutakuwa na ajira pindi watakapomaliza masomo yao.
